
Na Boniphace John OKULY BLOG – DODOMA
WAKALA wa Barabara za Vijijini na Mijini Tanzania (TARURA) umewataka wananchi, wakandarasi na wadau wengine wa sekta ya ujenzi kutumia maabara zake zilizopo katika mikoa mbalimbali nchini, ili kuhakikisha ubora wa kazi na vifaa vinavyotumika katika ujenzi unazingatia viwango vinavyotakiwa.
Hayo yamesemwa Septemba 7, 2026, jijini Dodoma na Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Tafiti na Udhibiti wa Ubora wa TARURA, Mhandisi Vincent Lwanda, ambaye amesema mwitikio wa wadau wanaotumia huduma za maabara hizo unaendelea kuongezeka.

Mhandisi Lwanda amesema maabara hizo zina uwezo wa kufanya vipimo mbalimbali vya ubora wa vifaa vya ujenzi pamoja na tafiti zinazosaidia kuhakikisha miradi ya barabara na miundombinu mingine inatekelezwa kwa kuzingatia viwango vinavyotakiwa.
Aidha, amesema vipimo hivyo vinafanyika kwa kutumia miongozo na nyaraka za kitaalamu zinazotolewa na Wizara ya Ujenzi, huku mashine zinazotumika katika maabara hizo zikifanyiwa urekebishaji wa kitaalamu (calibration) kila mwaka na Shirika la Viwango Tanzania (TBS), hatua inayolenga kuhakikisha vipimo vinavyofanyika vinakuwa sahihi na vya kuaminika.
Katika hatua nyingine, TARURA imeonyesha mashine maalum ya kisasa ya uchimbaji inayotumika kufanya uchunguzi wa tabia na uimara wa udongo uliopo chini ya ardhi kabla ya utekelezaji wa miradi mikubwa ya ujenzi.
Kwa mujibu wa TARURA, mashine hiyo imegharimu takribani Sh bilioni mbili na ina uwezo wa kuchimba pamoja na kuchukua sampuli za udongo kutoka kina kirefu chini ya ardhi kwa ajili ya uchunguzi wa kitaalamu wa kijiolojia na kijiotekiniki.
Kwa upande wao, wanafunzi wanaopata mafunzo ya tafiti kwa vitendo katika maabara za TARURA wamesema uwepo wa vifaa vya kisasa unawapa fursa ya kujifunza zaidi na kuongeza ujuzi katika kufanya tafiti mbalimbali, licha ya kuwa bado wako katika hatua za masomo.
Mmoja wa wanafunzi hao, Bahati Mzuchi, amesema matumizi ya vifaa hivyo yamewasaidia kupata uelewa mpana wa namna tafiti zinavyofanyika kwa vitendo na kutambua mambo mbalimbali yanayohusiana na taaluma yao.
Amesema maabara hizo 17 za Tafiti na Udhibiti wa Ubora zilizopo katika maeneo mbalimbali nchini, ikiwemo maabara ya Dodoma, zinawajengea uwezo na kuwaandaa wanafunzi hao kwa ajili ya soko la ajira na utekelezaji wa majukumu yao ya kitaaluma baada ya kuhitimu masomo ya uhandisi.






No comments:
Post a Comment