RUWASA YAAGIZWA KUSHIRIKIANA NA SEKTA BINAFSI KUFIKISHA MAJI VIJIJI 1,575 - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Wednesday, September 9, 2026

RUWASA YAAGIZWA KUSHIRIKIANA NA SEKTA BINAFSI KUFIKISHA MAJI VIJIJI 1,575


NA Mwandishi Wetu – DODOMA


WAKALA wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) umetakiwa kushirikiana na Sekta Binafsi na wadau wengine katika kutafuta Sh trilioni tatu zitakazosaidia kukamilisha miradi ya maji katika vijiji 1,575 vilivyobaki nchini.

Hatua hiyo inalenga kufanikisha azma ya Serikali ya kuhakikisha wananchi wote wanaoishi vijijini wanapata huduma ya maji safi na salama, huku RUWASA ikieleza kuwa inahitaji jumla ya Sh trilioni 5.1 kwa ajili ya kutekeleza miradi hiyo.

Kwa mujibu wa RUWASA, kwa sasa Wakala huo una uwezo wa Sh trilioni 2.06, hivyo kuna upungufu wa takribani Sh trilioni tatu ambao unatakiwa kupatikana kupitia ushirikiano na wadau mbalimbali, hususan Sekta Binafsi.

Ushauri huo umetolewa Septemba 9,2026 jijini Dodoma na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji, Mhandisi Rose Ambrose, ambaye pia ni mlezi wa RUWASA, wakati akifungua kikao kazi cha siku tatu cha Bodi ya Wakurugenzi, Menejimenti pamoja na Mameneja wa RUWASA wa Mikoa na Wilaya.

Mhandisi Rose amesema RUWASA inapaswa kutafuta njia mbadala za kupata fedha za kutekeleza miradi ya maji, ikiwemo kuimarisha ushirikiano na Sekta Binafsi.

«“RUWASA mnatakiwa kutafuta njia mbadala wa kupata fedha za kutekeleza miradi hiyo na hivyo mnatakiwa kushirikiana na Sekta Binafsi,” amesema.»

Amesema Wizara ya Maji inaitegemea RUWASA pamoja na mameneja wa maji wa mikoa na wilaya kuhakikisha wananchi wanaendelea kuunganishwa na huduma ya maji na kufikisha kiwango cha upatikanaji wa huduma hiyo zaidi ya asilimia 85 ambacho tayari kimefikiwa.

“RUWASA umejipambanua kwa kutekeleza miradi ya maji na kufikisha huduma kwa zaidi ya asilimia 85 ya wananchi wanaoishi vijijini.

“Aidha, ili kuhakikisha kuwa huduma ya maji inawafikia watu wote waishio vijijini, Wizara imeielekeza RUWASA kuanza kutekeleza mpango wa kufikisha huduma ya maji katika vijiji 1,575 visivyokuwa na huduma hiyo,” amesema.


Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya RUWASA, Ruth Koya, amesema Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, amekuwa akisisitiza umuhimu wa Serikali kuhakikisha wanawake wanatuliwa mzigo wa kutembea umbali mrefu kutafuta maji.

Amesema kauli hiyo inapaswa kuwa chachu kwa RUWASA kuongeza kasi ya utekelezaji wa miradi ya maji vijijini ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma hiyo kwa urahisi.

Koya amewataka mameneja wa maji wa mikoa na wilaya kwenda kutekeleza mikakati na mipango ya Wakala huo kwa ufanisi, ili kusukuma mbele gurudumu la maendeleo kwa kuwafikishia wananchi huduma ya maji.


Naye Mkurugenzi Mkuu wa RUWASA, Wolta Kirita, amesema Wakala huo ulioanzishwa miaka saba iliyopita umepata mafanikio makubwa katika kuhakikisha huduma ya maji inawafikia wananchi wa vijijini.

Kirita amesema kutokana na juhudi hizo, vijiji vilivyobaki bila huduma ya maji vimepungua na kufikia 1,575.

“Katika kuhakikisha vijiji vyote vilivyobaki vinafikiwa na maji, zinahitajika Sh trilioni 5.1 lakini zipo Sh trilioni 2.06, hivyo zinatakiwa kutafutwa Sh trilioni tatu kutoka kwa wadau mbalimbali hasa Sekta Binafsi,” amesema.

Amesema fedha hizo zitatumika siyo tu kuanzisha miradi mipya, bali pia kukamilisha ujenzi wa miundombinu ya maji 858 ambayo inaendelea katika maeneo mbalimbali nchini.

Kwa upande wa miradi mipya, Kirita amesema RUWASA ilikuwa imepanga kuanza utekelezaji wa miradi 314, lakini Wakala huo umetakiwa kuongeza idadi hiyo hadi miradi 400, hatua inayolenga kupunguza zaidi idadi ya vijiji ambavyo havina huduma ya maji.

Amesema kikao kazi hicho cha siku tatu kitajadili na kuweka maazimio yatakayosaidia kuongeza kasi ya utekelezaji wa miradi hiyo, pamoja na kubaini njia mbadala za kupata fedha za kugharamia miradi ya maji.

Kirita amesema ushirikiano kati ya RUWASA, Sekta Binafsi na wadau wengine ni muhimu katika kuhakikisha azma ya Serikali ya kuwafikishia wananchi wote wa vijijini huduma ya maji safi na salama inafikiwa.

No comments:

Post a Comment