Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Mhe. Wanu Hafidh Ameir, Septemba 23, 2026 jijini Arusha, amekutana na kuzungumza na wanufaika 50 wa mpango huo, wanaoendelea na kambi maalum ya mafunzo katika Taasisi ya Afrika ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela (NM-AIST).
Mhe. Wanu amewasisitiza wanufaika hao kutumia fursa hiyo kwa kujifunza kwa bidii, kudumisha nidhamu na kujenga misingi imara ya maarifa na ujuzi itakayowawezesha kufikia malengo yaliyokusudiwa na kuwa wataalamu watakaotoa mchango katika maendeleo ya Taifa.
Kwa upande wake, Makamu Mkuu wa NM-AIST, Prof. Maulilio Kipanyula, amesema wanufaika hao watapatiwa mafunzo mbalimbali kwa kipindi cha miezi 10, yakiwemo yanayolenga kujenga uzalendo na kuwaandaa kwa mazingira ya taaluma na kazi. Amesema tayari wamefanyiwa screening test ya kubaini uwezo wao katika lugha ya Kiingereza na Hesabu, hatua itakayosaidia kutambua maeneo yanayohitaji msaada zaidi katika ujifunzaji.
Akizungumza kwa niaba ya wanufaika, Lewis Mwasha na Laurencia Thobias wameishukuru Serikali kwa kuendelea kutoa fursa za ufadhili wa masomo kwa vijana wenye ndoto na kuwapa nafasi ya kujenga uwezo katika maeneo yenye umuhimu kwa maendeleo ya Taifa.
Wamesema watatumia kikamilifu fursa hiyo kwa kujifunza kwa bidii, kuzingatia nidhamu na kutumia maarifa watakayoyapata kuleta matokeo chanya katika jamii, huku wakitambua kuwa uwekezaji unaofanywa na Serikali katika elimu, sayansi na teknolojia ni sehemu muhimu ya kuwaandaa vijana kushiriki katika uchumi wa sasa na wa baadaye.











No comments:
Post a Comment