SANGU: MSITUMIE UCHAGUZI KUGAWANYA TALGWU - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Thursday, September 17, 2026

SANGU: MSITUMIE UCHAGUZI KUGAWANYA TALGWU


Na Okuly Julius, OKULY BLOG , DODOMA 


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Ajira na Mahusiano ), Mhe. Deus Sangu, amewataka wajumbe wa Mkutano Mkuu wa Uchaguzi wa Chama cha Wafanyakazi wa Serikali za Mitaa Tanzania (TALGWU) kuhakikisha uchaguzi huo unafanyika kwa amani, utulivu na kuheshimu Katiba ya chama, akisisitiza kuwa uongozi ni utumishi na si kutawala.

Sangu ameyasema hayo leo Septemba 17, 2026 jijini Dodoma wakati akifungua rasmi Mkutano Mkuu wa Uchaguzi wa TALGWU, ambapo amewataka viongozi watakaochaguliwa kusikiliza kero za wanachama na kuzitatua kwa uadilifu.

Akirejea maandiko matakatifu ya Marko 10:45 na Mathayo 20:26-27, Sangu amesema viongozi wanapaswa kutambua kuwa uongozi ni nafasi ya kuwahudumia wengine na si kujiona kuwa ni wakubwa kuliko wanaowaongoza.

Amesisitiza kuwa uchaguzi huo usitumike kama chanzo cha migawanyiko ndani ya TALGWU, bali uwe fursa ya kuimarisha umoja na mshikamano wa chama.

Sangu amewapongeza viongozi na wanachama wa TALGWU kwa kudumisha amani, utulivu na ushirikiano ndani ya chama, akieleza kuwa utulivu wa chama hicho una mchango katika utulivu wa Serikali na Taifa kwa ujumla.

Aidha, amesema Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan inatambua na kuthamini haki za wafanyakazi, huku akieleza kuwa milango ya Ofisi ya Waziri Mkuu ipo wazi kupitia mfumo wa majadiliano (Social Dialogue) katika kushughulikia changamoto za watumishi.

Ametaja baadhi ya changamoto hizo kuwa ni stahiki za uhamisho, malimbikizo ya madeni na masuala mengine yanayohusu maslahi ya watumishi.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa TALGWU, Tumaini Nyamhokya, amepongeza ushirikiano uliopo kati ya chama hicho na Serikali, akisema mawasiliano ya karibu na viongozi wa Serikali yamesaidia kupunguza migogoro na kuleta tija kwa watumishi.

Nyamhokya amemshukuru Waziri Sangu kwa kuendelea kuwa msikivu katika masuala yanayowahusu wafanyakazi, akisema ushirikiano kati ya Serikali na TALGWU ni muhimu katika kutafuta ufumbuzi wa changamoto zinazowakabili watumishi.

Amesema vikao mbalimbali vya chama, ikiwemo Kamati ya Utendaji na Baraza Kuu, vimefanyika kwa amani na utulivu mkubwa, hali ambayo amesema inaonesha mazingira mazuri kuelekea uchaguzi wa viongozi.

Nyamhokya pia ameeleza kuwa TALGWU itaendelea kusimama ndani ya shirikisho la vyama vya wafanyakazi katika kulinda haki na maslahi ya watumishi nchini.

Mkutano huo umehudhuriwa na viongozi na wawakilishi wa vyama vya wafanyakazi kutoka Kenya, Somalia na Malawi, pamoja na viongozi wastaafu wa TALGWU, akiwemo Katibu Mkuu Mstaafu Rashid Mtega.



Akizungumza katika Mkutano Mkuu huo, Kaimu Katibu Mkuu wa TALGWU, Wandiba Ngocho, amewasilisha changamoto sita zinazowakabili watumishi wa Serikali za Mitaa, huku akiiomba Serikali kuzitafutia ufumbuzi ili kuboresha mazingira ya kazi, maslahi ya wafanyakazi na utoaji wa huduma kwa wananchi.

Ngocho amesema changamoto hizo ni pamoja na ucheleweshaji wa fedha za likizo, ucheleweshaji wa malipo ya posho na leseni za huduma kwa baadhi ya watumishi wa kada za afya, stahiki za uhamisho, utekelezaji wa mfumo wa PEPMIS, miundo ya utumishi na mchakato wa kubadilishiwa kada (re-categorization), pamoja na kutofanya kazi kwa ufanisi kwa baadhi ya Mabaraza ya Wafanyakazi.

Amesema baadhi ya watumishi hupokea stahiki za likizo kwa awamu au baada ya muda uliopangwa, huku changamoto nyingine ikiwa ni kuchelewa kwa malipo ya stahiki za uhamisho kwa watumishi wanaohamishwa kutoka kituo kimoja cha kazi kwenda kingine.

Kuhusu mfumo wa PEPMIS, Ngocho amesema kuna changamoto katika utekelezaji na matumizi yake, hivyo ameiomba Serikali kuendelea kufanya maboresho yatakayorahisisha matumizi ya mfumo huo kwa watumishi.

Ameeleza pia kuwa baadhi ya watumishi hukumbana na vikwazo katika mchakato wa kubadilishiwa kada kulingana na elimu na ujuzi walioupata.

Aidha, TALGWU imeomba kuboreshwa kwa utendaji wa Mabaraza ya Wafanyakazi katika halmashauri na taasisi, ili kuongeza ushirikishwaji wa wafanyakazi katika masuala yanayohusu ajira na mazingira yao ya kazi.

Ngocho amezipongeza jitihada zinazofanywa na Serikali ya Awamu ya Sita katika kusikiliza na kushughulikia changamoto za wafanyakazi, huku akisisitiza umuhimu wa kuimarisha zaidi majadiliano kati ya Serikali na wafanyakazi.

Waziri Sangu amehitimisha kwa kuwatakia wajumbe uchaguzi mwema na wenye mafanikio, akiwataka watakaoshinda na ambao hawatachaguliwa kushirikiana baada ya uchaguzi kwa ajili ya kujenga TALGWU moja yenye nguvu na mshikamano.


No comments:

Post a Comment