Na Boniphace John, Dodoma
SERIKALI imeagiza ukarabati na urejeshaji wa miundombinu ya Soko la Machinga Dodoma iliyoharibiwa na moto kukamilishwa ndani ya siku 10, ili kuwawezesha wafanyabiashara walioathirika kurejea katika shughuli zao za kujipatia kipato.
Aidha, Serikali imezitaka taasisi mbalimbali, ikiwemo taasisi za fedha na Halmashauri ya Jiji la Dodoma, kuendelea kuwaunga mkono wafanyabiashara walioathirika kwa kuwawezesha kupata mitaji na kuendelea na shughuli zao baada ya janga hilo.
Kauli hiyo imetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Mhe. Rosemary Senyamule, wakati alipofika katika Soko la Wamachinga Dodoma kutoa taarifa kuhusu chanzo cha moto huo pamoja na tamko la Serikali kufuatia tukio lililotokea Septemba 20, 2026.
Senyamule amesema chanzo cha moto huo ni hitilafu katika mfumo wa umeme iliyosababishwa na uunganishaji wa umeme usiozingatia viwango, ambapo nyaya ziligusana juu ya vizimba vilivyojengwa kwa mbao katika eneo la Block C.
Amesema baadhi ya wafanyabiashara walikuwa wameunganisha mifumo ya umeme wa sola na umeme wa TANESCO, jambo ambalo ni kinyume na taratibu za kiusalama na linaweza kusababisha mifumo hiyo kutofanya kazi kwa usalama na hatimaye kupelekea majanga ya moto.
Kutokana na hali hiyo, Senyamule amewataka wafanyabiashara wa soko hilo na wananchi kwa ujumla kuepuka kuunganisha umeme kiholela na kuhakikisha kazi zote za ufungaji na uunganishaji wa umeme zinafanywa kwa kuzingatia viwango na taratibu za usalama zilizowekwa na mamlaka husika.
Pia amesisitiza umuhimu wa maboresho katika ujenzi wa vizimba vya biashara, akieleza kuwa ujenzi huo unapaswa kuzingatia viwango vya kitaalamu ili kupunguza hatari ya moto na majanga mengine.
Senyamule amesema Serikali tayari imeunda timu ya haraka kwa ajili ya kufanya tathmini na kubaini miundombinu na vitu vilivyoathirika pamoja na hatua zinazopaswa kuchukuliwa ili wafanyabiashara waweze kurejea katika maeneo yao ndani ya siku 10.
Amesema baada ya hatua hiyo, Serikali itaunda timu nyingine kutoka kada mbalimbali kwa kushirikiana na uongozi wa soko, ambayo itakuwa na jukumu la kuhakikisha changamoto zilizopo zinafanyiwa maboresho na hazijirudii.
Timu hiyo itashughulikia maeneo mbalimbali ikiwemo mifumo ya umeme, usalama wa moto, ujenzi na mpangilio wa vizimba kwa lengo la kupunguza uwezekano wa kutokea kwa majanga kama hayo siku zijazo.
Katika hatua nyingine, Senyamule amewashukuru wananchi na taasisi mbalimbali zilizoshiriki katika kutoa taarifa na kuzima moto huo, akizitaja Jeshi la Zimamoto na Uokoaji pamoja na Jeshi la Polisi, ambalo lilihakikisha usalama wa mali za wafanyabiashara wakati zoezi la uzimaji moto likiendelea.
Aidha, amesema Ofisi ya Mkuu wa Mkoa kwa kushirikiana na Ofisi ya Mkuu wa Wilaya imeamua kuwapatia waathirika wa moto huo kifuta jasho cha Shilingi 500,000 kila mmoja, wakati wakisubiri kukamilika kwa ukarabati wa maeneo yao ndani ya siku 10.
Senyamule pia amesema kuna umuhimu wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma kuanza haraka ujenzi wa soko jingine la Wamachinga ili kupunguza msongamano wa wafanyabiashara katika soko hilo.
Amesema Halmashauri ya Jiji tayari imetenga Shilingi bilioni mbili katika bajeti ya mwaka wa fedha kwa ajili ya ujenzi wa soko hilo jipya.


No comments:
Post a Comment