
Na Mwandishi Wetu
DODOMA RS
Wakuu wa Taasisi za Umma na Binafsi pamoja na Halmashauri ya Jiji la Dodoma wametakiwa kurejea na kuzingatia Mwongozo wa Utekelezaji wa Shughuli za Usafi wa Mwisho wa Mwezi, wa mwaka 2016, ili kuimarisha utekelezaji wa usafi na kuongeza uwajibikaji katika ngazi zote.
Wito huo umetolewa leo na Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Mhe. Jabiri Shekimweri, wakati akishiriki zoezi la usafi wa mwisho wa mwezi lililofanyika katika Kata ya Kizota Relini, eneo la Barabara ya Singida, Jijini Dodoma.

Mhe. Shekimweri amesema mwongozo huo ni nyenzo muhimu katika kuongoza utekelezaji wa shughuli za usafi, hivyo ni muhimu kurejewa na kufikishwa katika ngazi zote za uongozi, ili kila mmoja afahamu wajibu wake na kushiriki kikamilifu katika kulinda usafi wa mazingira.
“Niwaombe kupitia mwongozo wa mwaka 2016 ili muimarishe usafi wa mwezi na kuhakikisha unafika katika ngazi zote za uongozi, ili kila mtu ajue wajibu wake,” amesema Mhe. Shekimweri.
Amesema mwongozo huo unaelekeza malengo ya usafi, madhara ya kutofanya usafi, utaratibu wa utekelezaji pamoja na mfumo wa ufuatiliaji, hatua ambazo zinaweza kusaidia kuongeza uwajibikaji na kuhakikisha zoezi la usafi linafanyika kwa ufanisi katika maeneo yote.
Akizungumzia usafi wa mazingira, Mhe. Shekimweri amewapongeza wananchi wa Kata ya Kizota Relini kwa mwitikio wao katika zoezi hilo, huku akiwataka kuacha kutupa taka kwenye mitaro inayotumika kupitisha maji ya mvua.
Amesema kuziba kwa mitaro kutokana na taka kunaweza kuzuia mtiririko wa maji na kusababisha maji kusambaa katika maeneo ya makazi, hivyo kuongeza hatari ya madhara wakati wa mvua.
“Mitaro ikiwa imezibwa kwa uchafu, maana yake maji yatashindwa kupita sehemu yake na kusambaa kwenye makazi ya watu na kuleta madhara makubwa,” amesema.
Ameongeza kuwa elimu kwa wananchi kuhusu matumizi sahihi ya mitaro ni muhimu ili kujenga uelewa kwamba mitaro ni kwa ajili ya kupitisha maji, si kutupia taka.
Kwa upande wake, Mkuu wa Kitengo cha Udhibiti wa Taka Ngumu na Usafi waMazingira, Ndugu Mkana Mohamed Mkana, amesema zoezi hilo limepata mwitikio mkubwa kutoka kwa wananchi, jambo lililowezesha usafi kufanyika kwa haraka na kwa ushirikiano.
Nao wananchi wameshukuru zoezi hilo kufanyika katika maeneo yao, wakisema limewakumbusha wajibu wao wa kufanya usafi kila siku na si kusubiri siku ya mwisho wa mwezi, pamoja na kuwapatia elimu kuhusu umuhimu wa kutunza mazingira.
Usafi wa mazingira ni wajibu wa kila mmoja. Kila taasisi, kila kaya na kila mwananchi ana nafasi katika kulinda usafi na mazingira ya Dodoma.












No comments:
Post a Comment