BENKI ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB), kwa kushirikiana na Benki ya Maendeleo ya Afrika Mashariki (EADB), imezindua dirisha maalum la uwezeshaji wa fedha lenye thamani ya Sh bilioni 50 kwa ajili ya kuwawezesha wakulima wadogo na wafanyabiashara katika minyororo ya thamani ya kilimo, mifugo na uvuvi nchini.
Dirisha hilo limewezeshwa kupitia mkopo wa Sh bilioni 50 kutoka EADB kwenda TADB, kwa lengo la kuongeza upatikanaji wa mitaji nafuu, kuchochea uwekezaji na kuongeza tija pamoja na thamani katika shughuli za uzalishaji na biashara.
Walengwa watawezeshwa kupata mikopo yenye masharti rafiki kwa ajili ya ununuzi wa pembejeo na zana za kisasa, uzalishaji, uchakataji, usindikaji, uhifadhi, usafirishaji na upatikanaji wa masoko.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mtendaji wa TADB, Frank Naybundege, amesema upatikanaji wa fedha nafuu ni muhimu katika kuongeza tija, uongezaji thamani na ushindani katika sekta za kilimo, mifugo na uvuvi.
Amesema TADB itahakikisha fedha hizo zinawafikia walengwa na kutumika katika shughuli zenye tija, huku uwekezaji ukizingatia mzunguko wa biashara na mahitaji ya uzalishaji.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa EADB, Bernard Mono, amesema ushirikiano huo unaonesha dhamira ya taasisi hiyo kupanua upatikanaji wa fedha za maendeleo na kuelekeza mitaji katika sekta zenye uwezo wa kuchochea ukuaji wa uchumi na kuongeza ajira.
Amesema kupitia ushirikiano huo, wakulima na wafanyabiashara wadogo wataweza kuongeza uzalishaji, thamani na ushindani wa bidhaa zao katika masoko ya ndani na nje.
Dirisha hilo linatarajiwa kuchochea uwekezaji vijijini, kupunguza utegemezi wa uuzaji wa bidhaa ghafi, kuongeza thamani ya mazao na bidhaa za mifugo na uvuvi, pamoja na kuimarisha ushiriki wa biashara ndogo katika minyororo ya thamani.
















No comments:
Post a Comment