TANZANIA NA KOREA ZATAFUTA USHIRIKIANO IMARA WA KIUCHUMI - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Friday, September 11, 2026

TANZANIA NA KOREA ZATAFUTA USHIRIKIANO IMARA WA KIUCHUMI



Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar (Mb), akiwa katika picha na Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Exim ya Korea Kusini Bw. Jeong-hwa Seo, baada ya kukutana pembezoni mwa Mkutano wa Mawaziri wa Ushirikiano wa Kiuchumi kati ya Korea na nchi za Afrika wa mwaka 2026 (KOAFEC), uliofanyika jijini Seoul, Jamhuri ya Korea Kusini.

Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar (Mb), (katikati), akiwa katika picha na Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Exim ya Korea Kusini Bw. Jeong-hwa Seo, na Mhe. Angella Kairuki (Mb.), Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, baada ya kukutana pembezoni mwa Mkutano wa Mawaziri wa Ushirikiano wa Kiuchumi kati ya Korea na nchi za Afrika wa mwaka 2026 (KOAFEC), uliofanyika jijini Seoul, Jamhuri ya Korea Kusini.

Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar ((Mb), (wa tatu kulia), akiwa katika picha na Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Exim ya Korea Kusini Bw. Jeong-hwa Seo (wa tatu kushoto), Mhe. Angella Kairuki (Mb., Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari wa pili kulia), Mhe. Noel Kaganda, Balozi wa Tanzania nchini Korea Kusini (wa pili kushoto), Bw. Mohammed Khamis Abdulla, Katibu Mkuu, Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari (kulia), Bw. Dong-Hyuk Lee, Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa EDCF, Kanda ya Afrika, Benki ya Exim ya Korea (kushoto), baada ya kukutana pembezoni mwa Mkutano wa Mawaziri wa Ushirikiano wa Kiuchumi kati ya Korea na nchi za Afrika wa mwaka 2026 (KOAFEC), uliofanyika jijini Seoul, Jamhuri ya Korea Kusini.


(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, WF, Seoul, Korea Kusini)


Na. Benny Mwaipaja


Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar (Mb), amesema kuwa Tanzania na Korea Kusini zimekubaliana kuongeza kasi ya utekelezaji wa ahadi iliyotelewa na nchi hiyo ya dola za Marekani bilioni 2.5 kwa Tanzania kwa ajili ya kutekeleza miradi muhimu ya kimkakati itakayochochea maendeleo na ukuaji wa uchumi wa nchi katika sekta mbalimbali ikiwemo miundombinu ya usafirishaji, teknolojia, utamaduni, viwanda na afya.

Mhe. Balozi Omar amesema hayo jijini Seoul, Korea Kusini, pembezoni mwa Mkutano wa Mawaziri wa Jukwaa la Ushirikiano wa Kiuchumi kati ya Korea na nchi za Afrika, KOAFEC, wakati alipoongoza ujumbe wa Tanzania katika Mkutano huo pamoja na Benki ya Exim ya Korea ambayo ni wakala wa ukelezaji wa mfuko wa ushirikiano wa maendeleo ya kiuchumi wa Korea (EDCF).

Alisema Tanzania inathamini ushirikiano wa maendeleo wa Korea, lakini alisisitiza haja ya kuboresha utekelezaji wa miradi iliyokubaliwa kwa pamoja chini ya mfuko wa EDCF, akibainisha kuwa ucheleweshaji kwa upande wowote unaweza kudhoofisha ahadi zilizotolewa.

Alitoa wito wa uratibu wa karibu zaidi na juhudi madhubuti za kushughulikia ucheleweshaji katika utekelezaji wa miradi, tafiti za upembuzi yakinifu, na usanifu wa kina wa kihandisi, ambapo alisema baadhi ya miradi imechukua miaka kadhaa kabla ya kuanza kutekelezwa.

Mazungumzo hayo yamefanyika kufuatia mkutano wa Mawaziri wa Ushirikiano wa Kiuchumi wa Afrika na Korea, ambapo pamoja na mambo mengine, walijadili ushirikiano katika eneo la akili Unde (AI) kwa ajili ya maendeleo ya Bara la Afrika.

Akizungumzia matokeo ya Mkutano huo, Mhe. Balozi Omar amebainisha kuwa pande zote mbili zimekubaliana kufuatilia kwa karibu miradi iliyoahidiwa katika ziara ya Rais Dkt. Samia mwaka 2024 nhini Korea Kusini, ikiwemo mradi wa kwanza unaotarajiwa kuanza utekelezaji wake hivi karibuni wa ujenzi wa Chuo Mahiri cha Tehama jijini Dodoma.

Miradi mingine iliyojadiliwa na kupatiwa ufumbuzi ni pamoja na:Ujenzi wa Kituo cha Kimataifa cha Mikutano na Maonesho Zanzibar, Ujenzi wa Hospitali ya Rufaa ya Binguni na mradi wa Uendelezaji wa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili.

Aliutaja mradi mwingine kuwa ni Ujenzi wa barabara ya Ifakara kuelekea Mahenge, inayohusiana na mradi wa uchimbaji wa madini ya graphite.

Kuhusu mradi wa ununuzi wa mabehewa ya treni kwa ajili ya reli ya SGR, pande zote mbili zimekubaliana kufanya mapitio ya pamoja ya gharama na wigo wa mradi ili kuhakikisha unatekelezeka kwa ufanisi.

Mazungumzo hayo yamehitimishwa kwa pande zote mbili kuahidi ushirikiano wa karibu ili kuhakikisha miradi yote iliyokubaliwa inakamilika kwa wakati.

Kwa upande wake, Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Angelah Kairuki, alisema kuwa kupitia Mkutano huo Tanzania imenadi fursa mbalimbali za uwekezaji katika teknolojia bunifu zitakazo chochea ukuaji wa uchumi wa nchi na kukuza ajira na mapato ya Serikali kupitia kodi.

Aliwakaribisha wekezaji wa Korea, wafanyabiashara wa Korea wanaojihusisha na masuala ya teknolojia pamoja na teknolojia nyingine za kidijitali, kuja kuwekeza Tanzania katika uwekezaji wa miundombinu ya kidijitali. Ikiwemo vituo vya kutunzia taarifa (data centers), kukuza na kupanua mtandao wa mawasiliano wa 5G, kukuza upatikanaji wa fiber, ujenzi wa miundombinu ya mawasiliano ikiwemo minara ya mawasiliano.

“Lakini pia nimewakaribisha kuwekeza katika sekta ya Serikali Mtandao, kuja kuona namna gani huduma muhimu wanaweza kushirikiana na wakala wetu wa Serikali mtandao na Wizara, kuboresha huduma mbalimbali zinazotolewa na kiserikali, hizo za kijamii, za kielimu, za afya na huduma nyingine mbalimbali kupitia mifumo ya kidijitali” alisema Mhe. Kairuki

Alisema kuwa amewakaribisha pia kuwekeza katika teknolojia mbalimbali zikiwemo fedha, afya na utabibu, teknolojia za kuweza kusaidia uzalishaji katika kilimo na mnyororo mzima wa thamani.

Mhe. Kairuki pia aligusia suala la upatikanaji wa mtaji kwa ajili ya Shirika la Mawasiliano la Taifa (TTCL), uwekezaji katika fiber, maduka ya TTCL na huduma za simu ambapo wawekezaji wameonyesha nia ya kuwekeza na kushirikiana na Tanzania.

“Kama tunavyofahamu Tanzania tumejaliwa kuwa na idadi kubwa ya vijana na tunachokitaka kutumia idadi hiyo ya wingi wa vijana wetu kuwa ni faida kwa Taifa, faida kwa uchumi. Na hiyo ndiyo dhamira na azma kubwa ya Mheshimiwa Rais kupitia Serikali anayoiongoza ya awamu ya 6 kuona namna gani tunachochea fursa hizo kuja nchini na ziweze kutoa ajira kwa wananchi wetu”. Aliongeza Mhe. Kairuki.

Katika Jukwaa la KOAFEC la Mwaka huu lililobeba kaulimbiu ya “Harnessing AI and Digital Infrastructure for Africa's Transformation” uliandaliwa na Wizara ya Fedha na Uchumi ya Korea, Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) na Korea Eximbank, uliwakutanisha Mawaziri wa Afrika wanaoshughulikia uchumi, fedha, Akioi Unde (Artificial Intelligence) na mageuzi ya kidijitali; viongozi wa AfDB; kampuni za Afrika; na washirika wa marndeleo wa kimataifa.

Lengo kuu la kukutana ni kujadiliana namna ya kutumia Akili Unde (Artificial Intelligence) na miundombinu ya kidijitali kuharakisha maendeleo ya Afrika kwa kuangazia uwekezaji, ufadhili wa maendeleo, ubunifu wa teknolojia na kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi kati ya Korea na nchi za Afrika.

No comments:

Post a Comment