
Tanzania na Urusi zimekubaliana kuimarisha ushirikiano katika sekta ya elimu, sayansi, teknolojia na ubunifu, kwa lengo la kuongeza fursa za mafunzo na kubadilishana ujuzi na teknolojia kati ya nchi hizo mbili.
Makubaliano hayo yamefikiwa jijini Dar es Salaam Septemba 29, 2026, katika kikao cha pamoja kati ya Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Mhe. Wanu Amer Hafidh, na ujumbe kutoka Urusi.
Ujumbe huo uliongozwa na Bw. Denis Agafonov, Mkuu wa Kurugenzi ya Uchambuzi katika Ofisi ya Rais wa Shirikisho la Urusi, akiambatana na Bw. Vadim Titov, Mkuu wa Kurugenzi ya Ushirikiano na Ubia wa Kimkakati katika ofisi hiyo.
Katika kikao hicho, pande hizo zilijadili na kukubaiana maeneo ya kuimarisha ushirikiano, ikiweo mahusiano kati ya taasisi za elimu, kuongeza fursa za ufadhili wa masomo kwa wanafunzi wa Kitanzania na kuanzisha programu za pamoja za shahada.
Maeneo mengine ya kuongeza ushirikiano yaliyojadiliwa ni pamoja na ubunifu, sayansi na teknolojia, pamoja na kuweka mikakati ya kuwezesha uhamishaji wa teknolojia baina ya nchi hizo mbili.
Naibu Waziri Wanu ameushukuru ujumbe huo kwa kutembelea Tanzania na kueleza dhamira ya Serikali ya kuendelea kuimarisha ushirikiano uliopo kati ya nchi hizo katika elimu, sayansi, teknolojia na ubunifu.
Ujumbe kutoka Urusi umeahidi kuendelea kushirikiana na Tanzania katika kuimarisha mahusiano na kutekeleza maeneo yaliyokubaliwa kwa manufaa ya nchi hizo mbili.












No comments:
Post a Comment