TANZANIA, FINLAND ZABADILISHANA UZOEFU UCHENJUAJI NA UONGEZAJI THAMANI MADINI - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Wednesday, September 30, 2026

TANZANIA, FINLAND ZABADILISHANA UZOEFU UCHENJUAJI NA UONGEZAJI THAMANI MADINI



PORI, FINLAND

Tanzania na Finland zimeendelea kuimarisha ushirikiano katika Sekta ya Madini kupitia kubadilishana uzoefu na utaalamu katika maeneo ya uchenjuaji, uyeyushaji, usafishaji wa metali na uongezaji thamani madini.

Ushirikiano huo umejikita katika kuongeza ujuzi na uwezo wa wataalam wa Tanzania katika usimamizi wa mnyororo wa thamani wa madini, hususan katika matumizi ya teknolojia za kisasa na endelevu zinazolenga kuongeza thamani ya madini yanayozalishwa nchini.

Septemba 29, 2025, ujumbe wa wataalam kutoka Wizara ya Madini Tanzania, kwa kushirikiana na Taasisi ya Utafiti wa Jiolojia Finland (GTK), ulikutana na uongozi na wataalam wa maabara ya Metso Corporation katika mji wa Pori nchini Finland.

Metso ni miongoni mwa kampuni zinazojihusisha na teknolojia na suluhisho za uchakataji wa madini, uchenjuaji, uyeyushaji na usafishaji wa metali, pamoja na teknolojia za kuboresha ufanisi na uendelevu katika shughuli za viwanda vya madini.

Akielezea umuhimu wa ziara hiyo, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Msafiri Mbibo, alisema Tanzania inalenga kuendelea kutekeleza sera ya kuongeza thamani ya madini nchini ili kuhakikisha rasilimali hizo zinachangia zaidi katika uchumi wa taifa.

Aliongeza kuwa, ziara hiyo nchini Finland inalenga kuwawezesha wataalam wa Tanzania kujifunza uzoefu na teknolojia zinazotumika katika uchenjuaji, uyeyushaji na uongezaji thamani madini, huku akieleza kuwa GTK imekuwa mshirika muhimu katika kuendeleza ushirikiano wa kitaalamu katika Sekta ya Madini.

Kwa upande wake, mwakilishi wa GTK alieleza kuwa ziara hiyo ni sehemu ya kuimarisha ushirikiano wa kitaalamu kati ya Tanzania na Finland, hususan katika utafiti, teknolojia na matumizi ya mbinu endelevu katika mnyororo wa thamani wa madini.

Ujumbe huo pia ulipata fursa ya kujifunza kuhusu uzoefu wa Finland katika shughuli za uchenjuaji na uyeyushaji madini, ikiwemo teknolojia zinazotumika katika uchakataji wa madini kama nikeli na shaba, pamoja na hatua za kuhakikisha shughuli hizo zinafanyika kwa ufanisi na kuzingatia mazingira.

Ziara hiyo ya kimkakati imehusisha wataalam kutoka Wizara ya Madini na taasisi mbalimbali, ikiwemo Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST), Tume ya Madini, Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), Chemba ya Migodi Tanzania na Baraza la Taifa la Usimamizi wa Mazingira (NEMC).

Kukamiika kwa ziara hiyo kunatarajia kuongeza uwezo wa wataalam wa Tanzania katika teknolojia za kisasa za uchakataji na uongezaji thamani madini, sambamba na kuimarisha jitihada za Serikali za kuhakikisha Tanzania inaongeza manufaa ya kiuchumi kutokana na rasilimali zake za madini.TANZANIA, FINLAND ZABADILISHANA UZOEFU UCHENJUAJI NA UONGEZAJI THAMANI MADINI

No comments:

Post a Comment