Na Mwandishi Wetu - Chamwino, Dodoma
Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) wilaya ya Chamwino imefungua barabara ya Manda–Mafurungu yenye urefu wa kilomita 25 hatua ambayo imebadili hali ya usafiri na usafirishaji kwa wananchi wa kijiji cha Mafurungu baada ya kukabiliwa na changamoto ya muda mrefu ya kutokuwa na barabara.
Akizungumza kuhusu maendeleo ya mradi huo, Meneja wa TARURA wilaya ya Chamwino Mhandisi Richard Sanga amesema, barabara hiyo imefunguliwa ikiwa ni jitihada za serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kuunganisha wananchi na kurahisisha shughuli za kiuchumi na kijamii.
Amesema TARURA wilaya ya Chamwino inahudumia mtandao wa barabara wenye urefu wa kilomita 1,297 huku ujenzi wa barabara ya Manda–Mafurungu ukiwa ni muhimu kwa wananchi wa vijiji vya Manda na Mafurungu kwa ajili ya kurahisisha upatikanaji wa huduma za afya na elimu, kupunguza gharama za usafiri na kufungua fursa za kiuchumi.
"Awali barabara hii haikuwepo kabisa lakini baada ya kupata fedha tumeweza kuifungua, mkandarasi tayari ameshafungua kilomita zote 25 huku kazi zinazoendelea ni ujenzi wa makalavati, uwekaji wa kifusi katika maeneo korofi na maandalizi ya uchongaji wa mifereji kwa ajili ya kudhibiti na kuondoa maji ya mvua barabarani", amesema.
Ameeleza kuwa kutokana na umuhimu wa barabara hiyo katika bajeti ya mwaka huu wa fedha wataweka changarawe katika baadhi ya maeneo korofi huku mpango wa mwaka ujao wa fedha ukiwa ni kuweka kifusi barabara yote na kumalizia makalavati ili kuhakikisha barabara inapitika kwa urahisi na kwa uhakika kipindi chote cha mwaka.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa kitongoji cha Machimbo, Bw. Mrisho Ally amesema kabla ya barabara hiyo wananchi wa Mafurungu wakitaka kusafiri hadi Dodoma mjini safari ya kwenda na kurudi walikuwa wakitumia nauli zaidi ya Sh. 100,000/= hali iliyowalazimu kutumia muda mwingi na gharama kubwa.
Amesema kwa sasa gharama hiyo imeshuka hadi Sh. 24,000/= kwa safari ya kwenda na kurudi huku magari yakiwa yanafika moja kwa moja kijijini ambapo imepunguza gharama na muda wa usafiri.
Ameongeza kuwa eneo hilo lina shughuli kubwa za uchimbaji wa madini ya dhahabu zinazochangia uchumi wa wilaya ya Chamwino hivyo ameiomba serikali kuendelea kuboresha barabara hiyo ili iweze kutoa huduma kwa wananchi na wafanyabiashara katika kipindi cha mwaka mzima.
Naye, Bw. Zabroni Matonya mkazi wa Mafurungu na mwekezaji katika shughuli za uchimbaji madini amesema, barabara hiyo imekuwa mkombozi kwa wachimbaji na wawekezaji kutokana na kurahisisha usafirishaji wa vifaa na malighafi kwani awali ubovu wa barabara uliwafanya kutumia muda mrefu kusafirisha malighafi zao mjini hivyo ameishukuru serikali kwa barabara hiyo.
Mkazi wa Mafurungu Bi. Salma Mtacha amesema kabla ya barabara wanafunzi walikuwa wakitembea umbali mrefu kufika shuleni hali iliyokuwa ikiwatia hofu wazazi lakini sasa barabara imefunguka wanafunzi wanafika shuleni bila shida pia wananchi wanafika katika vituo vya afya na hospitali bila changamoto jambo ambalo limeongeza usalama na ustawi wa jamii.
Naye, Selemani Bundala mkazi wa Mafurungu amesema awali safari ya kutoka kijijini hadi Dodoma mjini kwa pikipiki ilikuwa ikigharimu hadi Sh. 100,000/= lakini baada ya barabara kufunguliwa hali imebadilika na mabasi sasa yanafika moja kwa moja kijijini.
Amesema wananchi wanathamini jitihada za serikali katika kufungua barabara hiyo na ameomba kazi ya uboreshaji iendelee hadi barabara hiyo iweze kupitika mwaka mzima.







No comments:
Post a Comment