Na Boniphace John, OKULY BLOG – DODOMA
Meneja wa Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini Tanzania (TARURA) Wilaya ya Dodoma, Mhandisi Emmanuel Mfinanga, amewataka wananchi kulinda miundombinu ya barabara na madaraja iliyopo na inayoendelea kujengwa, huku akiwataka kuchukua hatua za haraka kukabiliana na athari zinazoweza kusababishwa na mvua za El Niño.
Akizungumza Septemba 9, 2026, baada ya kufanya ziara ya ukaguzi wa barabara na madaraja yaliyojengwa katika maeneo ya Chigongwe, Ntyuka na Ihumwa jijini Dodoma, Mfinanga amesema kuna umuhimu mkubwa kwa kila mwananchi kuwa mlinzi wa miundombinu hiyo ili kuhakikisha inakuwa salama, imara na inatumika kwa muda mrefu.
Amesema baadhi ya miundombinu imekuwa ikiharibiwa na kuibiwa, ikiwemo betri za sola kwenye taa za barabarani pamoja na vyuma vya madaraja, hali ambayo amesema haikubaliki kutokana na gharama kubwa zinazotumika na Serikali katika ujenzi wake.
Mfinanga amewataka wananchi kuacha mara moja vitendo vya kuiba au kuharibu miundombinu, akisisitiza kuwa mwananchi yeyote atakayebainika kufanya vitendo hivyo ataripotiwa katika mamlaka husika, ikiwemo vituo vya Polisi vya kata au TARURA, kwa hatua za kisheria.
Aidha, amesema utupaji wa taka ovyo ni miongoni mwa sababu zinazochangia kuziba kwa mitaro na kusababisha maji kushindwa kutiririka vizuri wakati wa mvua, jambo ambalo linaweza kuleta athari katika makazi ya wananchi.
Kutokana na hali hiyo, amewataka wananchi kuacha kutupa taka ovyo na badala yake kushirikiana na viongozi wa kata, Halmashauri na Mkoa kufanya usafi katika maeneo yao ili kujiandaa mapema kabla ya kuanza kwa mvua za El Niño.
Mfinanga amesema TARURA itaendelea kupokea fedha zinazotolewa na Serikali kwa ajili ya kuboresha miundombinu iliyopo, kukamilisha miradi ambayo haijakamilika pamoja na kujenga miundombinu mipya katika maeneo ambayo bado hayajafikiwa.
Ametolea mfano eneo la Mkonze, ambapo amesema bado kuna makorongo mengi yanayohitaji kujengewa madaraja ili kuwawezesha wananchi kufika maeneo mbalimbali kwa urahisi, kwa muda mfupi na kwa gharama nafuu.
Kwa upande wake, Diwani wa Kata ya Chigongwe, William Nadoo, amesema ujenzi wa Daraja la Chigongwe umeondoa changamoto kubwa zilizokuwa zikiwakabili wananchi wa eneo hilo.
Amesema daraja hilo lililogharimu Sh milioni 606 lina urefu wa mita 36 na linaunganisha mitaa ya N’ghambala na Mkombola.
Kwa mujibu wa Nadoo, kabla ya ujenzi wa daraja hilo, wananchi walikuwa wakipata changamoto kubwa wakati wa mvua kutokana na mto kujaa maji, hali iliyokuwa ikikwamisha usafirishaji wa mazao hasa wakati wa mavuno.
Amesema changamoto hiyo pia ilikuwa ikiathiri wanafunzi ambao walishindwa kufika shuleni kwa wakati, lakini baada ya kukamilika kwa daraja hilo, hali hiyo imeondoka.
Nao baadhi ya wananchi wameeleza kufurahishwa na kuipongeza Serikali kwa utekelezaji wa mradi huo mkubwa wa Daraja la Chigongwe, wakisema umeleta mabadiliko katika shughuli zao za kila siku na za kiuchumi.
Isaya Juma, mkazi wa Mtaa wa N’ghambala, amesema kabla ya ujenzi wa daraja hilo wananchi walishindwa kufanya shughuli zao za kiuchumi kwa ufanisi kutokana na changamoto ya kuvuka kwenda upande wa pili wa mto.
Amesema hali hiyo ilikuwa ikiathiri shughuli za biashara, ikiwemo kwenda kwenye minada kutafuta masoko ya bidhaa na mifugo, akitolea mfano Mnada wa Kigwe uliopo Wilaya ya Bahi.
Amesema kukamilika kwa daraja hilo kumewawezesha wananchi kuvuka kwa urahisi na kuendelea na shughuli zao za kiuchumi bila vikwazo vilivyokuwepo awali.










No comments:
Post a Comment