TCU YAWATAKA WALIOPATA NAFASI VYUO ZAIDI YA KIMOJA KUJITHIBITISHA - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Tuesday, September 8, 2026

TCU YAWATAKA WALIOPATA NAFASI VYUO ZAIDI YA KIMOJA KUJITHIBITISHA



NA OKULY JULIUS, OKULY BLOG - DODOMA


Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) imewataka waombaji waliodahiliwa katika chuo zaidi ya kimoja kuthibitisha udahili wao katika chuo kimoja pekee, kuanzia leo Septemba 8 hadi 21, 2026, ili kukamilisha mchakato wa udahili wa Shahada ya Kwanza kwa mwaka wa masomo 2026/2027.

Akizungumza leo Septemba 8, 2026 jijini Dodoma, Katibu Mtendaji wa Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU), Prof. Charles Kihampa, amesema uthibitisho huo utafanyika kwa kutumia namba maalum ya siri iliyotumwa kwa waombaji kupitia ujumbe mfupi wa simu au barua pepe walizotumia wakati wa kuomba udahili.

Prof. Kihampa amesema waombaji waliodahiliwa katika vyuo zaidi ya kimoja wanapaswa kujithibitisha katika chuo kimoja pekee, huku wale watakaopata changamoto wakati wa mchakato huo wakitakiwa kuwasiliana na vyuo walivyodahiliwa kwa ajili ya kupata msaada wa haraka.

Aidha, amewataka waombaji kufuata maelekezo na taratibu zilizowekwa na vyuo pamoja na TCU ili kuepuka kupoteza taarifa zao za udahili.

Wakati huo huo, TCU imetangaza kuanza kwa Awamu ya Pili ya udahili wa Shahada ya Kwanza kwa mwaka wa masomo 2026/2027, kuanzia Septemba 8 hadi 21, 2026.

Waombaji ambao hawakuweza kutuma maombi au hawakupata nafasi katika Awamu ya Kwanza kutokana na sababu mbalimbali wametakiwa kutumia fursa hiyo kutuma maombi katika vyuo wanavyovipendelea.

Katika Awamu ya Kwanza, jumla ya waombaji 149,645 walituma maombi ya kujiunga na vyuo 93 vilivyoidhinishwa kudahili wanafunzi wa Shahada ya Kwanza.

TCU imesema nafasi za udahili kwa mwaka 2026/2027 zimeongezeka hadi 227,555, kutoka nafasi 205,652 mwaka 2025/2026, ikiwa ni ongezeko la nafasi 21,903, sawa na asilimia 10.7.

Aidha, jumla ya waombaji 117,334, sawa na asilimia 78.4 ya waombaji wote, wamepata udahili katika vyuo walivyoomba, huku idadi hiyo ikitarajiwa kuongezeka katika Awamu ya Pili.

No comments:

Post a Comment