TPDC YACHANGIA ZAIDI YA BILIONI 208 SERIKALINI KUPITIA KODI, MRABAHA NA GAWIO - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Monday, September 21, 2026

TPDC YACHANGIA ZAIDI YA BILIONI 208 SERIKALINI KUPITIA KODI, MRABAHA NA GAWIO

Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), Bw. Mussa Makame, akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma, Septemba 21, 2026, katika Ukumbi wa Idara ya Habari – MAELEZO, kuhusu utekelezaji wa Shirika hilo katika kipindi cha mwaka wa fedha 2025/26 na mwelekeo wa 2026/27.

Na OKULY JULIUS, OKULY BLOG, DODOMA


Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), Bw. Mussa Makame, amesema Shirika hilo limepata faida ya Shilingi bilioni 72.98 katika mwaka wa fedha 2025/26, huku likichangia zaidi ya Shilingi bilioni 208 katika mapato ya Serikali kupitia kodi, mgawo wa faida, mrabaha na gawio.

Makame amesema hayo leo Septemba 21, 2026, jijini Dodoma wakati akizungumza na Waandishi wa Habari kuhusu utekelezaji wa mwaka wa fedha 2025/26 pamoja na mwelekeo wa Shirika hilo katika mwaka wa fedha 2026/27.

Amesema katika kipindi hicho, TPDC imelipa Shilingi bilioni 50.04 kwa Serikali kupitia kodi, huku Shilingi bilioni 142.61 zikitolewa kama mgawo wa faida na mrabaha katika mfuko wa mapato ya mafuta na gesi.

Aidha, amesema TPDC imelipa gawio la Shilingi bilioni 15.118, hatua ambayo imeongeza mchango wa Shirika katika mapato ya Serikali.

Akizungumzia uzalishaji wa gesi asilia, Makame amesema TPDC kwa kushirikiana na waendeshaji wa Vitalu vya Songosongo na Mnazi Bay imeendelea kuzalisha wastani wa futi za ujazo milioni 170 za gesi kwa siku.

Amesema sehemu kubwa ya gesi hiyo inatumika katika uzalishaji wa umeme, huku nyingine ikitumika na viwanda, taasisi pamoja na majumbani.

Kuhusu Mradi wa Bomba la Mafuta Ghafi la Afrika Mashariki (EACOP), Makame amesema utekelezaji wa mradi huo umefikia asilimia 92.7, huku Tanzania kupitia TPDC ikiwa inamiliki asilimia 15 ya mradi huo.

Amesema mradi huo umezalisha takribani ajira 10,000, ambapo ajira 7,500 sawa na asilimia 75 zimetolewa kwa Watanzania.

Makame amesema pia zaidi ya kampuni 200 za Kitanzania zimepata kandarasi za kusambaza bidhaa na huduma zenye thamani ya zaidi ya Shilingi trilioni 1.325, huku Serikali ikiwa imekusanya zaidi ya Shilingi bilioni 100 kupitia kodi, ada, ushuru na tozo mbalimbali zinazohusiana na mradi huo.

Akizungumzia Kitalu cha Mnazi Bay, amesema visima viwili vipya vya kuongeza uzalishaji vina uwezo wa pamoja wa kuzalisha takribani futi za ujazo milioni 65 za gesi kwa siku.

Amesema utekelezaji wa mradi huo umegharimu Dola za Marekani milioni 90 na umehusisha kampuni 35 za Kitanzania.

Kwa upande wa Kitalu cha Ruvuma katika eneo la Ntorya, Makame amesema ujenzi wa bomba la gesi kutoka Ntorya hadi Madimba umefikia asilimia 67, huku mradi huo ukiwa na thamani ya Shilingi bilioni 122.7.

Amesema bomba hilo lenye urefu wa kilometa 34.2 litakuwa na uwezo wa kusafirisha hadi futi za ujazo milioni 140 za gesi kwa siku.

Aidha, amesema TPDC inaendelea na shughuli za utafutaji wa mafuta na gesi katika Kitalu cha Lindi-Mtwara kupitia uchukuaji wa taarifa za mitetemo ya 3D katika eneo lenye ukubwa wa takribani kilometa za mraba 736.

Kwa mujibu wa Makame, mradi huo una thamani inayokadiriwa kufikia Shilingi bilioni 107 na utekelezaji wake umefikia asilimia 50.

Akizungumzia matumizi ya gesi majumbani na viwandani, amesema TPDC imefanikiwa kuunganisha nyumba 1,000 katika mikoa ya Pwani na Lindi, pamoja na viwanda viwili na vituo vitatu vya CNG vinavyomilikiwa na wawekezaji binafsi.

Makame amesema katika mwaka wa fedha 2026/27, TPDC itaendelea kuongeza uzalishaji wa gesi asilia, kuendeleza miradi ya Ruvuma na Ntorya, kukamilisha ujenzi wa bomba la Ntorya-Madimba pamoja na kuimarisha shughuli za utafutaji wa mafuta na gesi katika maeneo mbalimbali nchini.

Amesema hatua hizo zinalenga kuongeza uzalishaji wa nishati, mapato ya Serikali na fursa za kiuchumi kwa Watanzania, sambamba na kuhakikisha rasilimali za mafuta na gesi zinatumika kuchochea maendeleo ya Taifa.
Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), Bw. Mussa Makame, akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma, Septemba 21, 2026, katika Ukumbi wa Idara ya Habari – MAELEZO, kuhusu utekelezaji wa Shirika hilo katika kipindi cha mwaka wa fedha 2025/26 na mwelekeo wa 2026/27.

No comments:

Post a Comment