UPIMAJI WA MACHO WAWEZA KUONGEZA MARADUFU MAPATO YA MAISHA YA MTOTO MTANZANIA - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Friday, September 25, 2026

UPIMAJI WA MACHO WAWEZA KUONGEZA MARADUFU MAPATO YA MAISHA YA MTOTO MTANZANIA



Na Mwandishi Wetu


Upimaji rahisi na wa kawaida wa macho pamoja na matumizi ya miwani unaweza kuongeza kwa zaidi ya mara mbili mapato ya maisha ya mtoto anayekulia Tanzania, huku wazazi wakihimizwa kuhakikisha watoto wao wanapimwa macho kabla ya kurejea shuleni kwa muhula mpya.

Matokeo mapya ya utafiti yaliyotolewa na Shirika la Kimataifa la Kuzuia Kupotea kwa Uwezo wa Kuona (IAPB) yanaonyesha kuwa Tanzania ni miongoni mwa nchi 23 duniani ambazo marekebisho ya mapema ya matatizo ya kuona yanaweza kuongeza mapato ya maisha ya mtoto kwa asilimia 124.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, sababu kuu ya watoto kutoona vizuri inahusishwa na matatizo ya macho ambayo hayajasahihishwa, hali inayoweza kuathiri uwezo wa mtoto kuona vizuri na kujifunza darasani.

Takwimu zinaonyesha kuwa tatizo hilo linasababisha watoto nchini Tanzania kupoteza jumla ya miaka 27,178 ya masomo shuleni, kutokana na changamoto zinazohusiana na uoni hafifu.

Hata hivyo, iwapo tatizo la kuona litagunduliwa mapema mtoto akiwa na umri wa miaka mitano na kusahihishwa kwa kutumia miwani inayofaa hadi atakapofikisha miaka 18, utafiti unaonyesha kuwa hatua hiyo inaweza kuongeza kwa asilimia 124 mapato ya maisha ya mtoto anayekulia Tanzania.

Kutokana na matokeo hayo, wataalamu wa afya ya macho duniani wamewahimiza wazazi wenye uwezo kuhakikisha watoto wao wanapata huduma za upimaji wa macho mara kwa mara, hususan kabla ya kuanza shule au kurejea shuleni baada ya likizo.

IAPB pia imezindua kampeni ya “Love Your Eyes Back-to-School” (Yapende Macho Yako Shule Zinapofunguliwa), inayolenga kuongeza uelewa kuhusu afya ya macho ya watoto kupitia ujumbe unaowafikia wanafunzi shuleni, darasani pamoja na taarifa fupi zinazoweza kupelekwa kwa wazazi na walezi.

Akizungumzia umuhimu wa hatua hiyo, Peter Holland, Afisa Mkuu Msimamizi wa IAPB, amesema upimaji wa macho na upatikanaji wa miwani unaweza kuwa miongoni mwa uwekezaji muhimu zaidi ambao mzazi anaweza kufanya kwa maisha ya baadaye ya mtoto.

“Upimaji rahisi na wa kawaida wa macho na miwani unaweza kuwa mojawapo ya uwekezaji bora zaidi wa mzazi kwa maisha ya baadaye ya mtoto wake,” amesema Holland.

Amesema baadhi ya wazazi wanaweza kushindwa kufanya mipango ya upimaji wa macho au kugharamia miwani, hivyo serikali zinapaswa kuhakikisha kila mtoto anapata fursa ya kufikiwa na huduma hizo.

“Kila mtoto anastahili kuona vizuri akiingia shuleni kwa mara ya kwanza ama akifungua shule kuanza muhula mpya baada ya likizo,” amesema.

Kwa upande wake, Sumrana Yasmin, Mkurugenzi wa Kifundi wa Afya Shirikishi katika Sightsavers, amesema kila mtoto anastahili kupata nafasi ya kuona, kujifunza na kushamiri, akisisitiza kuwa kuwekeza katika afya ya macho ya watoto ni hatua muhimu katika kufungua fursa zao.

Amesema lengo la upimaji wa macho na utoaji wa miwani si tu kuzuia kupotea kwa uwezo wa kuona, bali pia kuwawezesha watoto kutumia kikamilifu uwezo wao, kubadilisha maisha yao na kuhakikisha hakuna mtoto anayeachwa nyuma.

Naye Anadine Marshall, Mkurugenzi wa Miradi wa CharityVision International, amesema mtoto anayeshindwa kuona ubao darasani anaweza kutafsiriwa kimakosa kuwa hana uwezo wa kujifunza.

Amesema upimaji rahisi wa macho unaweza kugundua tatizo ambalo vinginevyo lingeweza kudumu kwa miaka mingi bila kutambuliwa.

Kwa mujibu wa Marshall, kuwafikia watoto shuleni na kuwapatia miwani pale inapohitajika kunaweza kuondoa kikwazo rahisi cha uoni hafifu ambacho kinaweza kuleta mabadiliko makubwa katika elimu, kujiamini, matumaini na maisha yao ya baadaye.

Wito huo wa IAPB umetolewa kuelekea Mkutano wa Dunia wa Wakuu wa Nchi kuhusu Afya ya Macho, unaotarajiwa kufanyika Antigua na Barbuda Novemba 2, ambapo wakuu wa nchi na wadau wataweka ahadi za kuimarisha huduma za afya ya macho duniani.

IAPB ni muungano wa kimataifa wa sekta ya afya ya macho unaojumuisha zaidi ya mashirika 250 katika zaidi ya nchi 100, yanayoshirikiana kuhakikisha watu wote wanapata huduma za afya ya macho.

Sightsavers ni shirika la kimataifa linaloshirikiana na serikali na wadau katika zaidi ya nchi 30 zenye kipato cha chini na cha kati barani Afrika na Asia, likilenga kukabiliana na upofu unaozuilika na changamoto za uoni hafifu, pamoja na kuboresha upatikanaji wa huduma za afya, elimu na ajira kwa watu wenye ulemavu.

No comments:

Post a Comment