WATUHUMIWA 441 WA MAKOSA MBALIMBALI YA UHALIFU WANASHIKILIWA NA JESHI LA POLISI MJINI MAGHARIBI - ZANZIBAR - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Saturday, September 26, 2026

WATUHUMIWA 441 WA MAKOSA MBALIMBALI YA UHALIFU WANASHIKILIWA NA JESHI LA POLISI MJINI MAGHARIBI - ZANZIBAR


Jeshi la Polisi Mkoa wa Mjini Magharibi katika misako na operesheni zilizofanyika kwa kipindi cha miezi miwili limefanikiwa kuwakamata watuhumiwa 441 kwa makosa mbalimbali ikiwemo makosa ya wizi wa pikipiki, unyang'anyi wa kutumia silaha, uvunjaji, udhalilishaji, dawa za kulevya na Pombe za kienyeji (Gongo).

Akizungumza na waandishi wa habari huko ofisini kwake Madema, Wilaya ya Mjini, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mjini Magharibi, Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Elthon P. Banzi, amesema katika operesheni hiyo walifanikiwa kukamata pikipiki 29 na bajaji ambazo ziliibiwa katika maeneo mbalimbali ya Mkoa huo na nje ya Mkoa. Hivyo amewataka wananchi kufika kituoni hapo ili kutambua pikipiki hizo.

Katika hatua nyingine, kupitia operesheni hizo zilifanikisha kuwakamata watuhumiwa watatu kwa kosa la kujifanya wafanyakazi wa serikali jambo ambalo ni kosa kisheria.

Watuhumiwa hao baada ya kufanyiwa upekuzi walipatikana na sare zinazofanana na Jeshi la Polisi Tanzania, Sare za Vikosi vya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, bunduki bandia yenye muundo wa Ak 47, bastola ya bandia, pingu, filimbi na vifaa vingine vinavyotumiwa na maafisa wa majeshi mbalimbali nchini.

Kamanda Banzi amewataja watuhumiwa hao ni Nassir Ahmed Salum, miaka 25, Mshirazi wa Fuoni Migombani na Haji Issa Faki, miaka 39, Mshirazi wa Kianga Domoni wilaya ya Mjini, na Zahran Masoud Zahran, miaka 24, Mshirazi wa Fuoni Wilaya ya Magharibi B Mkoa wa Mjini Magharibi.

Watuhumiwa wengine walikamatwa mnamo tarehe 26/08/2026 majira ya saa 2.00 usiku huko maeneo ya njia ya Miwani shehia ya Kizimbani wilaya magharibi A na Mkoa Mjini Magharibi, watuhumiwa watatu ambao ni (1) Saleh Jangiani Ibrahim maarufu Madenge, miaka 25, mshirazi wa sharifumsa. (2) Khamisi Haji Khamisi maarufu Kanji, miaka 38, mshirazi wa Mtoni na (3) Khamisi Majala Suleiman, miaka 27, mshirazi wa Magogoni wote kwa pamoja walimjeruhi na vitu vyenye ncha kali sehemu ya shingoni mtu aliyefahamika kwa jina la Hassani Khamisi Rashid, miaka 25, mshirazi wa Betras kisha kumnyang’aya pikipiki yake aina ya Tvs yenye namba za usajili M 980 ABN yenye thaman ya Tshs 3,5000,000/= jambo ambalo ni kosa kisheria. Watuhumiwa hao kupitia kwa mtuhumiwa Khamis maarufu Kanji alimkodi dereva huyo kisha kwenda kutekeleza uhalifu huo watuhumiwa wamefikishwa mahakamani kwa hatua zaidi msako mkali ulifanyika na kufanikiwa kuwakamata watuhumiwa hao na pikipiki hiyo.

Hata hivyo, amesema Jeshi la Polisi limeendelea na jitihada za kupunguza ajali za barabarani kwa kuhakikisha madereva wanatii sheria za usalama barabarani katika utekelezaji wa jukumu hilo Kamanda Banzi amesema walifanikiwa kukamata makosa 5497 yakihusisha magari, bajaji na pikipiki.

Aidha, katika kipindi hicho kumetokea ajali 15 ambapo kati ya hizo ajali 11 zimesababisha vifo vya watu 11 na ajali nne (04) zimesababisha majeruhi saba (07) Jeshi la Polisi limeendelea na mikakati ya kuhakikisha kwamba madereva wanatii sheria bila kushurutishwa.

Kamanda Banzi, ameeleza kwamba katika kipindi cha miezi miwili, Jeshi la Polisi lilifanikiwa kufikisha mahakamani mashauri 165 ambapo kati ya mashauri 77 yalipata hatia ambapo watuhumiwa walihukumiwa vifungo, kulipa fidia, faini na kifungo cha kati ya miaka 30 na miaka sita.

Aidha, Kamanda Banzi, amewataja baadhi ya watuhumiwa waliohukumiwa ni:-
Fahmi Makame Simai, miaka 33 mshirazi na mkazi wa Magogoni wilaya ya Magharibi ‘’B’’ alihukumiwa Kwenda Chuo cha Mafunzo miaka 30. Ali Khamis Ali, miaka 32 mshirazi na mkazi wa welezo Wilaya ya Mjini alihukumiwa Kwenda Chuo cha Mafunzo miaka 30.

Abdul Khamis Makenzi, miaka 30 mnyamwezi na mkazi wa Kisauni Wilaya ya Magharibi ‘’B’’ mtuhumiwa amehukumiwa kutumikia Chuo cha Mafunzo miaka 15 kwa kosa la kwanza na miaka 17 kwa kosa la pili na adhabu ziende sambamba, pia kulipa fidia kwa mhanga kiasi cha shilingi milioni moja, mtuhumiwa alimbaka na kumuingilia mtoto wa kike mwenye umri wa miaka 14.

Mtuhumiwa mwingine ni Abdulrahim Adam Haji, miaka 19 mshirazi na mkazi wa Tomondo wilaya ya Magharibi ‘’B’’ mtuhumiwa amehukumiwa kutumikia Chuo cha Mafunzo miaka 10 kwa kosa la kwanza na miaka 12 kwa kosa la pili na adhabu ziende sambamba, pia ametakiwa kulipa fidia kwa mhanga kiasi cha shilingi milioni moja, mtuhumiwa alimbaka na kumuingilia kinyume na maumbile mtoto mwenye umri wa miaka nane (08).

Kamanda Banzi, amepongeza ushirikiano uliopo kati ya Jeshi la Polisi na Wananchi wa Mkoa wa Mjini Magharibi ambapo kupitia mkutano huo amewaalika wananchi wote wa Mkoa wa Mjini Magharibi kushiriki matembezi ya pamoja yanayotarajiwa kufanyika Oktoba 03, 2026.






No comments:

Post a Comment