WAZIRI BASHIRU MGENI RASMI MKUTANO MKUU WA MVIWATA - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Monday, September 28, 2026

WAZIRI BASHIRU MGENI RASMI MKUTANO MKUU WA MVIWATA



Na Shua Ndereka, OKULY BLOG, Morogoro


Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mheshimiwa Balozi Dkt. Bashiru Ally Kakurwa, anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika kongamano la kitaifa la wakulima wadogo litakalofanyika Septemba 29 na 30 mwaka huu, mkoani Morogoro, kuelekea Mkutano Mkuu wa 31 wa Mtandao wa Vikundi vya Wakulima Tanzania (MVIWATA).

Kongamano hilo la siku mbili, linawapa wakulima fursa ya kujadili changamoto na fursa katika sekta ya kilimo, pamoja na kubadilishana uzoefu katika shughuli za uzalishaji.

Akizungumza na OKULY BlOG
, Mwenyekiti wa MVIWATA Taifa Apolo Chamwela, amesema Mkutano Mkuu wa mtandao huo ni takwa la Kikatiba linalowapa wanachama nafasi ya kutathmini yaliyofanyika, kujadili mwelekeo wa taasisi na kuchagua viongozi wa Bodi watakaoongoza MVIWATA kwa kipindi cha miaka mitatu, 2026 hadi 2029 ikiwa ni miongoni mwa agenda katika mkutano huo.

“Ukuaji wa MVIWATA umepitia vipindi vingi, katika milima na mabonde tangu kuanza kwake, ni kama ukuaji wa mtoto, safari hii ya miaka 31 ya MVIWATA tunajivunia mafanikio mengi yaliyopatikana katika safari ya mika 31, kama ujenzi wa masoko zaidi ya 11 nchi nzima ili kupunguza changamoto ya masoko kwa wakulima wadogo, kwa baadhi likiwemo soko la kimataifa la Kibaigwa Dodoma, soko la Nyandila, Kinole, Tawa mkoani Morogoro” amesema Chamwela.

Aidha Chamwela amesema mbali na mafanikio hayo MVIWATA inatarajia kujenga kiwanda cha uchakataji wa mazao ya viungo mkoani Morogoro na kuanzisha Benki ya wakulima wadogo kwa ajili ya kuwasaidia wakulima katika mitaji, mikopo, masoko na huduma mbalimbali za kifedha.

Hata hivyo MVIWATA imeendelea kuwa jukwaa la wakulima kujadili masuala yanayohusu uzalishaji, masoko, upatikanaji wa huduma na fursa mbalimbali za maendeleo ya kilimo huku mikutano hiyo ikiwa ni fursa kwa wakulima, kutoa maoni, kusikiliza uzoefu wa wenzao na kujadili kwa pamoja namna ya kuimarisha nafasi ya mkulima katika maendeleo ya kilimo.

Awali akitoa taarifa kwa wananchama wa MVIWATA, Mkurugenzi Mtendaji wa Stephen Ruvuga, amewataka wanachama kujitokeza kwa wingi katika kongamano hilo, ambalo litajadili mada ikiwemo uhakika wa ardhi kwa wakulima wadogo, kilimo ikolojia, uhuru wa chakula, haki ya uchumi na ushiriki wa wanawake na vijana.

Zaidi ya wanachama elfu moja kutoka Tanzania bara na Zanzibar wanatarajiwa kushiriki katika kongamano hilo la kitaifa la Wakulima wadogo na Mkutano Mkuu wa 31 wa MVIWATA, utakaofanyika Oktoba mosi, 2026, mkoani Morogoro.

2 comments:

  1. Makala nzuri sana, na Hongera kwa Mviwata.

    ReplyDelete
  2. Asante sana kwa kutujuza. Kazi nzuri

    ReplyDelete