WAZIRI MKUU Dkt. Mwigulu Nchemba, amewataka wanamipango, wachumi, na watendaji wote wa serikali kuongoza mageuzi ya kiuchumi kupitia utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 na Mpango wa Nne wa Maendeleo wa Miaka Mitano (2026/27–2030/31).
Waziri Mkuu ameyasema hayo leo (Alhamisi, Septemba 17, 2026) alipokuwa akifungua na kuhitimisha Kongamano la Wanamipango Tanzania lililofanyika katika kituo cha mikutano cha kimataifa cha Arusha (AICC) jijini Arusha, ambapo Waziri Mkuu amesisitiza kuwa kupitia utekelezaji wa Dira 2050 taifa limeingia katika awamu mpya ya utendaji kazi inayohitaji kasi, ujasiri, na utendaji wa "business unusual" (akimaanisha kufanya kazi bila mazoea) ili kufikia malengo yaliyowekwa.
"Tanzania imeanza rasmi utekelezaji wa Dira 2050 Julai Mosi, 2026, katika uzinduzi uliofanyika Julai 17. Lengo kuu ni kuijenga nchi kuwa na uchumi wenye thamani ya dola za Kimarekani trilioni moja na pato la mtu mmoja mmoja la dola 7,000 kwa mwaka ifikapo 2050."
"Ili kufikia matokeo hayo, lazima tufanye kazi kwa kasi, tuache mazoea na tubadili mtazamo hasi uliojengeka dhidi ya sekta binafsi kwamba wao sio wazalendo, wakati utekelezaji wa Dira 2050 unaitegemea sekta binafsi kwa asilimia 70," amesema Dkt. Mwigulu.
Ili kuchochea uwekezaji na ajira, Waziri Mkuu ameongeza msisitizo kwa kutoa wito wa kuipatia sekta binafsi heshima na fursa sawa na sekta ya umma ambapo amewataka wanamipango kutumia tafiti na taarifa sahihi kuingia kwenye mikataba ya ubia kati ya sekta ya umma na sekta binafsi (PPP) bila hofu.
Dkt. Mwigulu amewataka watendaji hao kuisaidia Serikali kujitegemea na kupanua wigo wa mapato ambapo amesema kutokana na kubadilika kwa mfumo wa rasilimali za kimataifa na kupungua kwa misaada na mikopo nafuu, kuna umuhimu wa nchi kupanua wigo wake wa mapato ya ndani na kutekeleza mapendekezo ya Tume ya Rais ya Mfumo wa Kodi ili kuongeza kujitegemea.
Aidha, amewahimiza wanamipango na watendaji wa Serikali kuoanisha Sera, Mipango, na Bajeti ili kuhakikisha miradi yote ya kielelezo inakamilika kwa wakati, kwa bajeti iliyopangwa, na kwa viwango vinavyotakiwa, huku wakiepuka kubadili mipango kiholela au kuongozwa na dharura.
"Ninakumbuka nikiwa Waziri wa Fedha, wizara zinapitishiwa bajeti wakati wa Bunge la bajeti, lakini ndani ya mwezi Julai tu wizara zinakuja kuomba kubadili vipaumbele kwa kuwa mambo wanayopaswa kuyafanya hayamo kwenye bajeti waliyoiomba na kupitishiwa na Bunge," amesisitiza Waziri Mkuu.
Waziri Mkuu amewataka wataalamu wa tathmini na ufuatiliaji kutobaki na ujuzi/mifumo peke yao, bali watoke na kwenda kusimamia na kufuatilia mipango na utekelezaji wa miradi kwa ujasiri katika ngazi zote, mikoa, wilaya, na halmashauri ili kuzuia dharura na matumizi mabaya ya rasilimali.
"Moja ya eneo ambalo bado hatujafanya vizuri ni hili la tathmini na ufuatiliaji. Kwenye hili, bado tuna kazi ya kufanya. Ufuatiliaji lazima ujikite katika kuhakikisha miradi ya kielelezo na mipango yote iliyowekwa inaleta matokeo yenye tija, inakamilika kwa wakati, na inazingatia bajeti pamoja na viwango vilivyopangwa," amehimiza Waziri Mkuu.
Awali, akimkaribisha Waziri Mkuu kuhutubia, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji, Prof. Kitila Mkumbo, alibainisha kuwa makongamano yajayo hayatakuwa tena ya kujadili mipango pekee, bali itajikita katika kutoa taarifa za matokeo halisi ya utekelezaji kwani Serikali imewezesha upatikanaji wa nyenzo zote za kisheria na kimkakati kwa wakati ili kuongoza nchi kwa miaka 25 ijayo.
Naye, Katibu Mkuu wa Ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji, ambaye pia ni Katibu Mtendaji wa Tume ya Taifa ya Mipango, Dkt. Tausi Kida, amesema kongamano hilo ambalo ni la pili tangu kuundwa upya kwa Tume ya Taifa ya Mipango mwaka 2023, limewakutanisha zaidi ya washiriki 1,300 kutoka mikoa yote 26 ya Tanzania Bara. Washiriki hao ni pamoja na wachumi, wataalamu wa takwimu, maafisa mipango, watafiti, watendaji kutoka wizara, sekretarieti za mikoa, mamlaka za serikali za mitaa, sekta binafsi, na wadau wa maendeleo, lengo likiwa ni kujenga jukwaa la kubadilishana uzoefu na kuimarisha mipango jumuishi.








No comments:
Post a Comment