Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Mheshimiwa Dkt. Rhimo Nyansaho (Mb), tarehe 10 Septemba 2026, amekutana na kufanya mazungumzo na Waziri wa Ulinzi na Uzalishaji wa Kijeshi na Amiri Jeshi Mkuu wa Jamhuri ya Kiarabu ya Misri, Mheshimiwa Luteni Jenerali Ashraf Salem Zaher, jijini El Alamein, Misri.
Mazungumzo hayo ya viongozi hao waandamizi yalilenga kujadili na kuimarisha maeneo mbalimbali ya ushirikiano baina ya Wizara za Ulinzi za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Jamhuri ya Kiarabu ya Misri, ambazo ni nchi rafiki zenye uhusiano wa muda mrefu na wa kihistoria.
Aidha, viongozi hao walijadili masuala mbalimbali ya kiulinzi na usalama, pamoja na utekelezaji wa mambo yaliyojadiliwa wakati wa ziara ya Rais wa Jamhuri ya Kiarabu ya Misri, Mheshimiwa Abdel Fattah el-Sisi, nchini Tanzania mnamo Julai 18, 2026, ambapo alifanya mazungumzo na mwenyeji wake, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Mazungumzo hayo yalisisitiza umuhimu wa kuendelea kuimarisha uhusiano na ushirikiano wa kiulinzi na kijeshi baina ya Tanzania na Misri, hususan katika maeneo yenye maslahi ya pamoja kwa manufaa ya mataifa hayo mawili.
Katika ziara yake nchini Misri, Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Mheshimiwa Dkt. Rhimo Nyansaho (Mb), pia alipata fursa ya kushiriki katika Maonesho ya Kimataifa ya Anga na Teknolojia za Anga za Juu ya El Alamein (EIAS), yanayofanyika jijini El Alamein, Misri.
Maonesho hayo yamewakutanisha viongozi waandamizi wa Serikali, Mawaziri wa Ulinzi, Wakuu wa Majeshi, viongozi wa mashirika na kampuni mbalimbali za kimataifa, wanazuoni pamoja na wataalamu kutoka sekta ya ulinzi na anga, kutoka zaidi ya nchi 60 duniani.
Ushiriki wa Tanzania katika maonesho hayo unaendelea kutoa fursa muhimu ya kubadilishana uzoefu, maarifa na teknolojia katika sekta ya ulinzi na anga, pamoja na kujenga na kuimarisha mahusiano ya kimkakati na wadau mbalimbali wa kimataifa katika maeneo yenye maslahi ya pamoja.





No comments:
Post a Comment