
Na Mwandishi Wetu
CHUO Kikuu cha Aga Khan kimekuja na Kikohozi Classifier, teknolojia inayotumia akili bandia (AI) kuchanganua sauti za kikohozi kwa lengo la kusaidia kubaini magonjwa ya mfumo wa upumuaji, ikiwamo Kifua Kikuu (TB), pumu na magonjwa sugu ya mapafu (COPD).
Akizungumza kuhusu ubunifu huo, Msimamizi wa Mradi na Profesa Mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Aga Khan, Dkt. Kahabi Isangula, amesema teknolojia hiyo imetengenezwa nchini Tanzania kwa lengo la kuwezesha uchunguzi wa magonjwa hayo kufanyika kwa urahisi, haraka na kwa gharama nafuu.
Amesema mfumo huo unalenga kutengeneza kifaa kisichohitaji kuingizwa ndani ya mwili wa mgonjwa na ambacho kinaweza kutumika katika vituo vya afya vya ngazi za chini na maeneo ya jamii, hivyo kuongeza fursa ya wananchi kupata huduma za uchunguzi.
Kwa mujibu wa Dkt. Isangula, watafiti wanatarajia kukusanya na kurekodi sauti za kikohozi za watu 30,000 kwa kutumia simu janja na vifaa maalumu vya kurekodia. Taarifa hizo zitatumika kujenga kanzidata kubwa ya sauti za kikohozi ambayo itasaidia katika uundaji wa mfumo wa AI.
Amesema mfumo huo utachanganua sifa mbalimbali zinazopatikana katika sauti ya kikohozi na kuzihusianisha na viashiria vinavyoweza kuonyesha uwepo wa TB, pumu au COPD, hatua inayotarajiwa kusaidia wataalamu wa afya katika mchakato wa uchunguzi.
Utekelezaji unafanyika kwa ushirikiano na Maabara ya Teknolojia Chipukizi za Afya (Emerging Technologies for Health) ya Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS) pamoja na Chuo Kikuu cha Warwick cha Uingereza, kwa ufadhili wa UK Research and Innovation (UKRI) kupitia Medical Research Council (MRC).
Dkt. Isangula amesema mpango huo umepitishwa na Wizara ya Afya pamoja na Programu ya Taifa ya Kudhibiti Kifua Kikuu na Ukoma, huku shughuli za utafiti zikifanyika katika maeneo ya Dar es Salaam, Dodoma, Shinyanga, Iringa na Kilimanjaro.
Ameongeza kuwa baada ya kukamilika kwa utafiti na uchambuzi wa taarifa, hatua inayofuata ni kutengeneza programu ya simu janja, Kikohozi App, itakayounganishwa na mfumo wa AI na kufanyiwa majaribio kabla ya kuanza kutumika kwa upana.
Kwa upande wake, Mtafiti Msaidizi kutoka Chuo Kikuu cha Aga Khan na Shule ya Uuguzi na Ukunga Kanda ya Afrika Mashariki (SONAM EA), Devotha Kibanga, amesema ukusanyaji wa sauti unahusisha wagonjwa wapya ambao hawajaanza kutumia dawa au walioanza matibabu ndani ya kipindi kisichozidi miezi mitatu.
Amesema wakati wa zoezi hilo, mgonjwa huombwa kukohoa huku sauti ikirekodiwa kwa simu janja.
Taratibu za usalama huzingatiwa, ikiwa ni pamoja na matumizi ya barakoa na usafishaji wa vifaa kwa sanitaiza baada ya zoezi.
Ukusanyaji wa sauti hizo ulianza Machi mwaka huu na unatarajiwa kuendelea hadi Septemba 2027, wakati mradi mzima ukitarajiwa kukamilika mwaka 2028. Katika kipindi hicho, watafiti wataendelea kukusanya na kuchambua taarifa pamoja na kuendeleza mfumo huo kwa ajili ya matumizi yanayokusudiwa.




No comments:
Post a Comment