
Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dodoma (DUWASA) imeendelea kuadhimisha Wiki ya Huduma kwa Wateja kwa kuwafikia wafanyabiashara katika Soko la Machinga na maeneo ya pembezoni mwa soko hilo jijini Dodoma, kwa lengo la kusikiliza changamoto zao na kuboresha utoaji wa huduma.
Zoezi hilo ni sehemu ya juhudi za DUWASA za kuwa karibu na wateja wake, kufahamu mahitaji yao na kupata maoni yatakayosaidia kuboresha huduma za majisafi na usafi wa mazingira, pamoja na kuendelea kuimarisha huduma za kidijitali.
Akizungumza wakati wa zoezi hilo, Afisa Huduma kwa Wateja wa DUWASA, Emmanuela Mbawara, amesema mwaka huu Mamlaka hiyo imelenga kuwafikia wateja katika maeneo yao ya biashara na makazi ili kusikiliza maoni yao na kuhakikisha huduma zinazotolewa zinakidhi mahitaji yao.
Amesema zoezi hilo limeiwezesha DUWASA kupokea maoni na changamoto mbalimbali kutoka kwa wateja, ambazo zitatumika katika kuboresha huduma na kuongeza ufanisi wa utoaji wa huduma kwa wananchi.
“Lengo letu ni kuwa karibu na wateja wetu, kusikiliza changamoto zao na kuboresha huduma tunazozitoa, ili wananchi wapate huduma bora za majisafi na usafi wa mazingira, ikiwemo huduma za majitaka,” amesema Mbawara.
Katika zoezi hilo, DUWASA pia imetoa elimu kwa wateja kuhusu umuhimu wa kulipa bili za maji kwa wakati, matumizi sahihi na yenye ufanisi ya maji, pamoja na utunzaji wa miundombinu ya maji na majitaka.
Mbawara amesema Wiki ya Huduma kwa Wateja imekuwa fursa muhimu kwa DUWASA kuwafikia wananchi moja kwa moja, kusikiliza maoni yao na kutoa elimu kuhusu huduma mbalimbali zinazotolewa na mamlaka hiyo.
Ameongeza kuwa DUWASA itaendelea kuwafikia wateja wake katika maeneo mbalimbali na kutumia maoni pamoja na changamoto wanazozitoa kama sehemu ya maboresho ya huduma za majisafi na usafi wa mazingira jijini Dodoma.









No comments:
Post a Comment