Jeshi la Polisi limewataka wananchi wanaomiliki silaha kinyume cha sheria kuzisalimisha kwa hiari kabla ya Oktoba 31, 2026, huku likionya kuwa baada ya muda huo litaanza operesheni ya nchi nzima ya kuwabaini na kuwachukulia hatua wanaomiliki silaha hizo.
Wito huo umetolewa jijini Dodoma na Mkuu wa Dawati la Elimu na Udhibiti wa Silaha, Kamishna Msaidizi wa Polisi Sebastian Madembwe kufuatia kampeni ya usalimishaji wa silaha haramu kwa hiari iliyozinduliwa Agosti 31, 2026 jijini Dodoma na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Patrobas Paschal Katambi.
Amesema kampeni hiyo ni sehemu ya mkakati wa kupunguza idadi ya silaha haramu katika jamii, ambazo zimekuwa zikitumika katika kutenda makosa mbalimbali ya jinai, ikiwemo unyang’anyi wa kutumia silaha, mauaji, vitisho na majeruhi.
"Kupitia Tangazo la Serikali lililotolewa Agosti 22, 2026, wananchi wanaomiliki silaha kinyume cha sheria wamepewa muda wa miezi miwili, kuanzia Septemba Mosi hadi Oktoba 31, 2026, kuzisalimisha bila kufikishwa kwenye vyombo vya sheria kwa makosa yanayohusiana na umiliki huo, kwa mujibu wa masharti ya msamaha huo,"amesema.
Pia, amewataka wananchi ambao bado wanamiliki silaha haramu majumbani mwao kutumia fursa hiyo kuzisalimisha katika vituo vya Polisi vilivyo karibu huku.
"Baada ya Oktoba 31, 2026, Jeshi la Polisi linatarajiwa kuendesha operesheni nchi nzima kwa ajili ya kuwasaka na kuwabaini watu watakaokuwa bado wanamiliki silaha kinyume cha sheria,"amesema.
Aidha, amesema hatua hiyo inalenga kuhakikisha silaha ambazo hazijasajiliwa au zinazomilikiwa kinyume cha sheria hazibaki mikononi mwa wananchi na kutumika kuhatarisha maisha na usalama wa jamii.
"Kwa baadhi ya wananchi, silaha hizo zinaweza kuwa zimehifadhiwa majumbani bila kutumika, lakini umiliki wa silaha ambao hauzingatii matakwa ya sheria bado unaweza kumuweka mhusika kwenye matatizo ya kisheria,"amesema.
Hatua hiyo, kwa mujibu wa Polisi siyo tu inalenga kuwaepusha wananchi na hatua za kisheria, bali pia inalenga kulinda familia zao na jamii kwa ujumla dhidi ya madhara yanayoweza kusababishwa na silaha hizo.


No comments:
Post a Comment