DARAJA LA BILIONI 2.9 LAJENGWA KATIKA MRADI WA BARABARA WA BILIONI 24 ( KIMARA - KINYEREZI) - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Saturday, October 3, 2026

DARAJA LA BILIONI 2.9 LAJENGWA KATIKA MRADI WA BARABARA WA BILIONI 24 ( KIMARA - KINYEREZI)


Serikali kupitia Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) inaendelea mradi wa ujenzi wa barabara ya Kimara - Kinyerezi yenye urefu wa kilomita 6.7, ukiwemo ujenzi wa daraja lenye thamani ya shilingi bilioni 2.9, pamoja na miundombinu mingine muhimu katika eneo hilo.

Mradi huo wenye thamani ya jumla ya shilingi bilioni 24.06 unahusisha ujenzi wa barabara kwa kiwango cha zege, ujenzi wa daraja, makalavati matano (box culverts), mitaro pamoja na uwekaji wa taa za barabarani.


Akizungumza wakati wa kutembelea na kukagua maendeleo ya utekelezaji wa mradi huo Waziri wa Ujenzi Masanja Kadogosa, amesema kuwa kazi inayofanyika ina umuhimu mkubwa kwa wananchi, hususan katika kulinda makazi na miundombinu iliyopo pembezoni mwa barabara.

Aidha, ameeleza kuwa katika gharama ya jumla ya shilingi bilioni 24.06, ujenzi wa daraja pekee unagharimu shilingi bilioni 2.9, huku sehemu nyingine ya fedha ikitumika katika ujenzi wa barabara yenye urefu wa kilomita 6.7, Kingo, makalavati, mitaro na uwekaji wa taa za barabarani.

Amesema uwekezaji huo unaonesha dhamira ya Serikali ya kuhakikisha fedha zinazotengwa kwa ajili ya miradi ya maendeleo zinatumika kwa ufanisi na kuleta thamani halisi kwa wananchi.

“Mheshimiwa Rais amekuwa akisisitiza kila wakati kwamba kila fedha ya Serikali iliyotumika lazima ionekane thamani yake. Hapa kuna kazi kubwa inayofanyika. Tunajenga barabara, tunajenga daraja, makalavati, mitaro, kingo na tunaweka taa za barabarani,” amesema Kadogosa.
Ameipongeza TANROADS pamoja na washauri elekezi kwa ubunifu katika usanifu wa mradi huo, akisema hatua hiyo imesaidia kupunguza gharama ambazo Serikali ingelazimika kutumia katika fidia endapo nyumba za wananchi zingebomolewa.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Ilala Edward Mpogolo , ameeleza kuwa hivi karibuni Kamati ya Siasa ya Wilaya ilitembelea eneo la mradi na kupata maelezo kutoka TANROADS kuhusu utekelezaji wake, ambapo wajumbe walipongeza jitihada zinazofanywa na Serikali kupitia TANROADS katika kuboresha miundombinu.

Amesema ni muhimu wananchi kupata taarifa sahihi kuhusu miradi inayotekelezwa na Serikali ili kuepusha upotoshaji kuhusu gharama na kazi zinazotekelezwa.

Awali akitoa taarifa ya Maendeleo ya Mradi huo Mhandisi Mkazi Eng. Allan Shula amesema hadi sasa Mradi huo umefikia 58% ya utekelezaji wake.

No comments:

Post a Comment