WAZIRI MKUU, Dkt. Mwigulu Nchemba, amesisitiza umuhimu wa kurasimisha taratibu za ushirikiano katika shughuli za uchimbaji wa madini kwa kutumia mikataba rasmi, akisema hatua hiyo itasaidia kuweka wazi makubaliano ya pande zinazohusika na kuzuia migogoro.
Dkt. Mwigulu ametoa kauli hiyo leo, Jumamosi, Oktoba 3, 2026, wakati akizungumza katika hafla ya kufunga Maonesho ya Tisa ya Teknolojia ya Madini yaliyofanyika mkoani Geita.
“Twende tuanze kuhamia huku tukiendelea kuaminiana, lakini tuanze kurasimisha taratibu zetu za ushirikiano tunapofanya shughuli hizi za uchimbaji. Wizara imejitahidi mpaka sasa kuweka mikataba, twendeni tutumie mikataba na masharti ya mikataba yale yaliyowekwa,” amesema.
Amesema katika shughuli za uchimbaji zinazohusisha wawekezaji, wenye leseni na wamiliki wa maeneo, makubaliano ya ushirikiano yanapaswa kuwekwa katika mikataba ili kuweka utaratibu wa wazi wa namna pande hizo zitakavyoshirikiana.
Dkt. Mwigulu amesema Serikali itaendelea kusimamia sekta ya madini kwa ushirikiano wa wadau mbalimbali, akisisitiza umuhimu wa kuhakikisha rasilimali za madini zinawanufaisha Watanzania na jamii zinazozunguka maeneo ambako shughuli za uchimbaji zinafanyika.
Amesema Serikali imeweka utaratibu wa kuelekeza asilimia 10 ya makusanyo yatokanayo na madini kwenye utafiti wa kina wa rasilimali madini, akisisitiza umuhimu wa kuongeza utafiti ili Taifa liwe na uelewa mpana wa rasilimali zilizopo.
Dkt. Mwigulu amesema amepokea hoja na maoni mbalimbali yaliyotolewa na wadau katika maonesho hayo, ikiwemo masuala yanayohusu uwajibikaji kwa jamii na miradi ya maendeleo, na kwamba atayafikisha Serikalini kwa ajili ya kufanyiwa kazi kwa mujibu wa taratibu.
Awali, Waziri wa Madini, Antony Mavunde, amesema sekta ya madini inachangia asilimia 10.3 ya Pato la Taifa, huku wachimbaji wadogo wakichangia asilimia 40 ya uzalishaji wa madini nchini.
Mavunde amesema Tanzania Geological Survey imefanya utafiti wa kijiolojia katika asilimia 16 pekee ya eneo la nchi, hivyo Serikali imeelekeza sehemu ya mapato ya sekta ya madini kutumika kuongeza utafiti wa rasilimali zilizopo nchini.
Amesema mwaka uliopita Serikali ilikusanya Sh. trilioni 1.39 kutoka kwenye sekta ya madini na kwamba kwa mwaka huu lengo ni kukusanya Sh. trilioni 1.40. Katika robo ya kwanza ya mwaka, amesema Serikali ililenga kukusanya Sh. bilioni 351 na imekusanya Sh. bilioni 411, sawa na asilimia 117 ya lengo.
Mavunde pia amesema Serikali imeanza kupitia leseni kubwa za madini ambazo hazijaendelezwa, na kwamba hatua za kuzifuta zitaanza kuchukuliwa. Amesema eneo la Sitarike mkoani Katavi ni miongoni mwa maeneo yaliyoanza kushughulikiwa, ambapo maeneo yatakayoachwa yatapelekwa kwa wachimbaji wadogo.
Kwa upande wake, Rais wa Shirikisho la Vyama vya Wachimbaji wa Madini Tanzania (FEMATA), John Bina, ameipongeza Serikali kwa hatua mbalimbali inazochukua katika kuwawezesha wachimbaji wadogo na kuimarisha sekta ya madini.
Bina amesema Benki Kuu ya Tanzania imeendelea kununua dhahabu kutoka nchini na kwamba hadi sasa imekusanya zaidi ya tani 35 za dhahabu. Ameomba benki ziendelee kutoa mikopo kwa wachimbaji ili kuwawezesha kuongeza uzalishaji.
Aidha, amesisitiza umuhimu wa kuimarisha taarifa za kijiolojia na kuchukua hatua dhidi ya taarifa za uongo za kijiolojia zinazoweza kuwapotosha wachimbaji, pamoja na kuendelea kulinda madini ya Tanzanite.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa AngloGold Ashanti–Geita Gold Mining (GGML), Ashraf Suryaningrat, amesema kampuni hiyo itaendelea kushirikiana na Serikali katika kuendeleza ujuzi na vipaji vya Watanzania, biashara na mnyororo wa ugavi wa ndani, teknolojia, ubunifu na maendeleo ya jamii zinazozunguka mgodi.
Maonesho ya Tisa ya Teknolojia ya Madini yamefanyika mkoani Geita yakiwa na kaulimbiu “Madini ni Utajiri, Tuwajibike kwa Pamoja Kufikia Dira ya Taifa 2050.”
Katika maonesho hayo, jumla ya washiriki 1,052 walishiriki, ikilinganishwa na washiriki 400 katika maonesho yaliyopita.






No comments:
Post a Comment