
Na Okuly Julius, OKULY BLOG, DODOMA
Uwekezaji wa zaidi ya TSh bilioni 88 katika miradi ya majisafi jijini Dodoma unatarajiwa kuboresha upatikanaji wa huduma hiyo kupitia uchimbaji wa visima vinne vipya na ujenzi wa matanki mawili yenye uwezo wa kuhifadhi jumla ya lita milioni sita.
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Mhe. Rosemary Senyamule, amesema hayo Oktoba 19, 2026, jijini Dodoma wakati wa ziara yake ya kukagua miradi mbalimbali ya maendeleo, ikiwemo miradi ya majisafi na majitaka inayotekelezwa katika mkoa na Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dodoma (DUWASA)
Ameshukuru na kumpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kutoa fedha zinazowezesha utekelezaji wa miradi hiyo, akisema uwekezaji huo ni hatua muhimu katika kuboresha huduma za maji na usafi wa mazingira kwa wananchi wa Dodoma na maeneo jirani.
Kwa mujibu wa taarifa ya utekelezaji wa miradi hiyo iliyosimwa na Mkurugenzi wa Usambazaji Maji na Usafi wa Mazingira DUWASA, Mhandisi Bernard Rugayi, amesema DUWASA inaendelea kutekeleza miradi ya majisafi na majitaka kwa lengo la kukidhi mahitaji yanayoongezeka, hususan katika mji wa Serikali Mtumba na maeneo ya pembezoni.
Katika mradi wa maji safi, kazi zinazotekelezwa ni pamoja na uchimbaji wa visima vinne vipya, ujenzi wa tenki lenye uwezo wa kuhifadhi lita milioni tano na tenki jingine lenye uwezo wa kuhifadhi lita milioni moja kwa ajili ya kuimarisha usambazaji wa maji.
Uwekezaji huo unakuja wakati ambapo mahitaji ya maji jijini Dodoma yanafikia lita milioni 169 kwa siku, huku uzalishaji ukiwa lita milioni 88.8 kwa siku, sawa na takribani asilimia 53 ya mahitaji yote.
Hali hiyo inaonesha umuhimu wa kuongeza uzalishaji wa maji na kuboresha miundombinu ya usambazaji ili kupunguza pengo lililopo kati ya mahitaji na upatikanaji wa huduma hiyo muhimu.
MRADI WA MAJITAKA WAFIKIA ASILIMIA 50
Katika upande wa majitaka, DUWASA inaendelea kutekeleza ujenzi wa mabwawa 10 ya majitaka, ambapo kazi ya uchimbaji imekamilika kwa asilimia 100, huku ujenzi wa kuta za pembeni ukiendelea.
Akisoma taarifa Mkurugenzi wa Usambazaji Maji na Usafi wa Mazingira DUWASA, Mhandisi Bernard Rugayi amesema Mradi huo umefikia asilimia 50 ya utekelezaji wake kwa ujumla, wakati ujenzi wa bomba kuu la kukusanya majitaka lenye urefu wa kilomita 15.9 ukiwa umefikia zaidi ya asilimia 20.
Miundombinu hiyo inalenga kukusanya majitaka kutoka mji wa Serikali Mtumba na maeneo ya jirani ili yatibiwe kabla ya kutumika tena kwa shughuli zinazofaa, ikiwemo kilimo cha umwagiliaji.
Amesema Mradi huo pia unahusisha ujenzi wa nyumba za wafanyakazi na maabara za kisasa zitakazotumika kupima ubora wa maji yaliyotibiwa, hatua inayolenga kuimarisha usimamizi wa majitaka na kulinda afya za wananchi pamoja na mazingira.
Serikali inaendelea kusimamia utekelezaji wa miradi hiyo ili ikamilike kwa wakati na kwa kuzingatia viwango vya ubora, huku ikitarajiwa kuwa na mchango mkubwa katika kuboresha huduma za maji safi na usafi wa mazingira kwa wakazi wa Dodoma na maeneo yanayozunguka mji wa Serikali Mtumba.











No comments:
Post a Comment