KADOGOSA ASISITIZA UWAJIBIKAJI NA USHIRIKIANO WIZARA YA UJENZI - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Friday, October 9, 2026

KADOGOSA ASISITIZA UWAJIBIKAJI NA USHIRIKIANO WIZARA YA UJENZI


Waziri wa Ujenzi, Mhe. Masanja Kadogosa, amewataka watumishi wa Wizara ya Ujenzi kufanya kazi kwa bidii na kwa ushirikiano ili kufikia malengo ya Wizara na kuchangia maendeleo ya Taifa.

Akizungumza katika kikao kilichofanyika leo, Oktoba 9, 2026, katika Chuo cha Uongozi cha Mwalimu Julius Nyerere, Kibaha, mkoani Pwani, Waziri Kadogosa amesema kila mtumishi ana wajibu wa kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi na kuhakikisha kazi anazozifanya zinaleta tija kwa Taifa.

“Mimi nimekuja kufanya kazi, ni wajibu wenu pia kama watumishi wa Wizara kuhakikisha mnajituma na mnashirikiana, mnafanya kazi kwa bidii na kutambua kuwa nafasi ya Wizara hii katika maendeleo ya Taifa ni kubwa mno,” amesema Kadogosa.

Aidha, Waziri Kadogosa ameitaka Wizara kuangalia kwa mapana namna ya kupunguza msongamano wa magari na mizigo barabarani ili kupata suluhu ya changamoto zinazowakabili watumiaji wa barabara, hususan katika majiji makubwa nchini.

Vilevile, amesisitiza umuhimu wa uwajibikaji katika matumizi ya fedha za Serikali na zile zinazotolewa na wadau wa maendeleo, akielekeza fedha hizo kuelekezwa katika miradi ya ujenzi na ukarabati wa miundombinu kama ilivyokusudiwa.

Kadogosa amewahimiza washiriki kutumia kikao hicho kujadili changamoto zinazokabili Wizara na taasisi zake, pamoja na kuweka mikakati ya kupata suluhu zitakazowezesha kufikiwa kwa malengo yaliyowekwa.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Balozi, Mhandisi Aisha Amour, amesema kikao hicho kimeandaliwa kwa lengo la kuongeza ari na morali kwa watumishi, kuimarisha uwajibikaji na kuongeza tija na ufanisi katika utekelezaji wa majukumu yao.

Kikao hicho kimewashirikisha Menejimenti ya Wizara ya Ujenzi, Wakuu wa Taasisi zilizo chini ya Wizara pamoja na watumishi wa Wizara hiyo.








No comments:

Post a Comment