MADAKTARI BINGWA BMH WAHITIMISHA KAMBI MALAWI, WAGONJWA 64 WAFANYIWA UPASUAJI - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Friday, October 9, 2026

MADAKTARI BINGWA BMH WAHITIMISHA KAMBI MALAWI, WAGONJWA 64 WAFANYIWA UPASUAJI



Na Jeremiah Mbwambo, Lilongwe – Malawi


Madaktari bingwa kutoka Hospitali ya Benjamin Mkapa (BMH) nchini Tanzania wamehitimisha kambi ya matibabu ya kibingwa nchini Malawi, iliyowanufaisha wagonjwa zaidi ya 810, ambapo 64 wamefanyiwa upasuaji na wengine 49 kupewa rufaa ya kupata matibabu zaidi katika Hospitali ya Benjamin Mkapa.

Akizungumza wakati wa kufunga kambi hiyo, Katibu Mkuu wa Utawala wa Wizara ya Afya na Usafi wa Mazingira ya Malawi, Bw. Bestone Chisamile, amesema Hospitali ya Benjamin Mkapa imetekeleza kwa vitendo ushirikiano wa huduma za matibabu ya kibingwa kati ya Tanzania na Malawi.

Amesema nchi hizo mbili zimeanza majadiliano yatakayolenga kutathmini manufaa ya kambi hiyo kwa wagonjwa na kuweka msingi wa kurasimisha ushirikiano mpana zaidi katika huduma za matibabu, mafunzo ya wataalamu, upatikanaji wa dawa na rufaa za wagonjwa.

“Ushirikiano wa afya kati ya Malawi na Tanzania unatekelezwa kupitia kambi hii ya matibabu ya kibingwa. Majadiliano yetu yataangazia manufaa ya kambi hiyo kwa wagonjwa pamoja na umuhimu wa kurasimisha ushirikiano mpana zaidi,” amesema Chisamile.

Ameongeza kuwa madaktari na wataalamu kutoka Tanzania wamechangia kuimarisha ujuzi wa wataalamu wa Malawi kupitia utoaji wa huduma na kubadilishana uzoefu katika Hospitali ya Mzuzu na Hospitali ya Kamuzu iliyopo Lilongwe.

Kwa upande wake, Balozi wa Tanzania nchini Malawi, Mhe. Agnes Kayola, amesema kambi hiyo imekuwa na manufaa kwa wagonjwa na wataalamu wa afya wa nchi zote mbili, hasa katika upatikanaji wa huduma za kibingwa na kubadilishana uzoefu wa kitaaluma.

Kayola amesema kati ya wagonjwa zaidi ya 810 walionufaika na huduma zilizotolewa katika kambi hiyo, 64 wamefanyiwa upasuaji, huku wagonjwa 49 wakipewa rufaa ya kwenda Hospitali ya Benjamin Mkapa nchini Tanzania kwa matibabu zaidi.

Ameeleza kuwa mbali na huduma za matibabu, kambi hiyo imetoa fursa kwa wataalamu wa afya wa Tanzania na Malawi kujifunza na kubadilishana uzoefu katika fani mbalimbali, hatua inayochangia kuimarisha uwezo wa utoaji wa huduma za afya katika nchi hizo.

Kambi hiyo ilianza Septemba 28, 2026, na kuhitimishwa Oktoba 9, 2026, ikiwa ni sehemu ya ushirikiano unaohusisha Hospitali ya Benjamin Mkapa (BMH), SOTAC na Bohari ya Dawa (MSD).

Katika kambi hiyo, timu ya Tanzania imetumia magari maalumu ya kisasa yenye vyumba vya upasuaji, yanayowezesha utoaji wa huduma za matibabu katika mazingira mbalimbali.

Kambi hiyo ni sehemu ya juhudi za kuimarisha ushirikiano wa sekta ya afya kati ya Tanzania na Malawi, kupanua upatikanaji wa huduma za kibingwa na kuongeza ujuzi kwa wataalamu wa afya wa nchi hizo mbili.




No comments:

Post a Comment