DKT. LEKASHINGO AITAKA MADINI SACCOS KUONGEZA WANACHAMA, KUIMARISHA UWEKEZAJI - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Friday, October 9, 2026

DKT. LEKASHINGO AITAKA MADINI SACCOS KUONGEZA WANACHAMA, KUIMARISHA UWEKEZAJI



Na Mwandishi Wetu - DODOMA


Mwenyekiti wa Tume ya Madini, Dkt. Janet R. Lekashingo, ameitaka Madini SACCOS kuongeza idadi ya wanachama, kuimarisha uwekezaji na kuzingatia uwazi, uaminifu na nidhamu katika usimamizi wa fedha ili kufikia hadhi ya SACCOS ya Daraja B.

Akifungua kikao cha wanachama wa Madini SACCOS kilichofanyika Oktoba 9, 2026, katika Makao Makuu ya Tume ya Madini jijini Dodoma, Dkt. Lekashingo amesisitiza umuhimu wa kupanua wigo wa wanachama, kutoa elimu kwa watumishi ambao bado hawajajiunga na chama hicho, hususan katika Ofisi za Maafisa Madini Wakazi wa Mikoa, kuongeza hisa na kuimarisha uwekezaji.

Ameeleza kuwa mafanikio ya chama yanahitaji usimamizi madhubuti wa fedha, uwajibikaji na mipango inayotekelezeka, akizitaka Bodi na Menejimenti kuhakikisha kuwa juhudi za kufikia Daraja B zinaambatana na mikakati thabiti na utekelezaji wenye tija.

Awali, Mlezi wa Madini SACCOS ambaye pia ni Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini, Mhandisi Ramadhani Lwamo, amewataka viongozi wa chama hicho kuimarisha umoja miongoni mwa wanachama, kusimamia fedha kwa ufanisi na kuhakikisha wanachama wananufaika na huduma na uwekezaji unaofanywa kupitia chama hicho.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Madini SACCOS, Endrewcus Masero, amesema tangu kuanzishwa kwa chama hicho mwaka 2023, idadi ya wanachama imeongezeka kutoka 375 hadi 631 kufikia Septemba 2026, sawa na ongezeko la zaidi ya asilimia 67.

Amesema chama hicho kimetoa mikopo yenye thamani ya takribani shilingi bilioni 2.55 kwa wanachama 439, huku akiba zikifikia zaidi ya shilingi bilioni 1.15. Aidha, mtaji wa chama umeongezeka kutoka shilingi milioni 22.40 hadi shilingi milioni 72.88, huku thamani ya hisa ikipanda kutoka shilingi milioni 18.65 hadi shilingi milioni 77.85.

Masero ameongeza kuwa Madini SACCOS imepata hati safi za ukaguzi kwa miaka mitatu mfululizo, hatua inayoonesha kuimarika kwa usimamizi wa fedha na utoaji wa huduma kwa wanachama.

Amebainisha kuwa mpango mkakati wa mwaka 2027/2028 unalenga kuongeza idadi ya wanachama hai hadi wasiopungua 1,050, kufikisha mtaji wa chama angalau shilingi milioni 200 na kuimarisha utoaji wa huduma za kifedha kupitia mifumo ya kidijitali.

Amewahimiza wanachama kuongeza akiba na hisa zao, kutumia mikopo kwa malengo yaliyokusudiwa na kurejesha mikopo kwa wakati ili kuimarisha uwezo wa chama kutoa huduma zaidi.

Amesisitiza kuwa kufikia Daraja B kutahitaji ushirikiano wa karibu, uwazi, nidhamu na uwajibikaji kutoka kwa wanachama, Bodi, Menejimenti na uongozi wa Tume ya Madini.






No comments:

Post a Comment