KAMATI YA MIUNDOMBINU YARIDHISHWA NA MAENDELEO YA UJENZI WA BARABARA ZA AFCON ARUSHA - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Saturday, October 24, 2026

KAMATI YA MIUNDOMBINU YARIDHISHWA NA MAENDELEO YA UJENZI WA BARABARA ZA AFCON ARUSHA


Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu imeridhishwa na kasi ya utekelezaji wa miradi ya ujenzi wa barabara zinazohusishwa na maandalizi ya michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) jijini Arusha, huku ikisisitiza umuhimu wa miradi hiyo kukamilika kwa wakati na kwa kuzingatia viwango vya ubora.

Akizungumza leo Oktoba 24, 2026, jijini Arusha, wakati wa ziara ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa barabara hizo, Makamu Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mhe. Aboubakar Asenga, ameipongeza Wizara ya Ujenzi na Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) kwa hatua zilizofikiwa na kuwataka wasimamizi wa miradi kuhakikisha kazi zinakamilika kwa wakati uliopangwa.

Amesisitiza kuwa kasi ya utekelezaji inapaswa kwenda sambamba na ubora wa kazi, akieleza kuwa barabara hizo zitaendelea kuwa mali ya Watanzania na kutumika hata baada ya kukamilika kwa michuano ya AFCON.

“Hakikisheni barabara hizi zinakamilika kwa ubora na kwa wakati. Barabara hizi ni mali ya Watanzania hata baada ya mashindano ya AFCON, hivyo ubora wa kazi unapaswa kupewa kipaumbele sambamba na kasi ya utekelezaji,” amesema Mhe. Asenga.

Aidha, Kamati imeielekeza Wizara ya Ujenzi, viongozi wa Serikali ya Mkoa na Wilaya pamoja na wasimamizi wa miradi kuimarisha ufuatiliaji wa karibu ili kuhakikisha utekelezaji unazingatia masharti ya mikataba. Pia, imesisitiza umuhimu wa kutatua changamoto zinazowakabili wananchi wanaoishi katika maeneo yanayopitiwa na miradi hiyo.


Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Ujenzi, Mhandisi Godfrey Kasekenya, amesema Serikali imejipanga kuhakikisha barabara zinazohusishwa na maandalizi ya AFCON zinakamilika kwa wakati ili kuboresha miundombinu ya usafiri, kupunguza msongamano wa magari na kuimarisha mandhari ya jiji la Arusha.

Amezitaja barabara hizo kuwa ni barabara inayotoka katikati ya jiji la Arusha kuelekea Uwanja wa Ndege wa Arusha na kuendelea hadi Kisongo, yenye urefu wa kilomita 9.1, ambayo inapanuliwa kuwa na njia nne, pamoja na barabara ya Mbauda/Tanganyika Packers hadi Losinyai yenye urefu wa kilomita 70.

Amesema Serikali itaendelea kumsimamia mkandarasi ili kuhakikisha kazi zinafanyika kwa kasi inayotakiwa na kwa kuzingatia viwango vilivyowekwa, akibainisha kuwa maeneo ya kimkakati ya barabara hizo yanalengwa kukamilika kabla ya Machi 2027.

Vilevile, amewahimiza wakazi wa Arusha kushiriki katika kuboresha mandhari ya jiji kwa kupendezesha nyumba na maeneo yao ili kulifanya jiji hilo livutie zaidi wageni watakaofika wakati wa michuano ya AFCON.

Ameongeza kuwa usimamizi wa miradi hiyo utaendelea kuimarishwa ili kuhakikisha ubora wa kazi unaendana na thamani ya fedha zinazotumika.

Utekelezaji wa miradi hiyo unatarajiwa kuboresha mtiririko wa magari jijini Arusha, kurahisisha usafiri na usafirishaji, kuchochea shughuli za kiuchumi, kuongeza fursa za ajira na kuimarisha sekta ya utalii mkoani humo. 

No comments:

Post a Comment