Na Mwandishi Wetu - DODOMA
Mbunge wa Jimbo la Nzega Vijijini na Mjumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, Neto Paul Kapalata, ameishauri Serikali kufanya mapitio ya muundo wa Wizara ya Madini na Sheria ya Madini ili kuendana na mabadiliko ya sekta hiyo na kutekeleza malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo hadi mwaka 2050 pamoja na Maono ya Wizara ya Madini hadi mwaka 2030.
Kapalata amesema mapitio hayo yanapaswa kuzingatia mafanikio na mapungufu yaliyopo, kwa lengo la kuimarisha usimamizi wa rasilimali madini na kuifanya sekta hiyo kuwa na mwelekeo mpana zaidi wa kibiashara, huku ikichangia maendeleo ya taifa na kuongeza ushindani ndani na nje ya nchi.
Amesema sekta ya madini, inayotambulika kwa kaulimbiu ya “Madini ni Maisha na Utajiri,” inapaswa kutazamwa kama sekta ya kimkakati ya maendeleo ya taifa, kwa kuzingatia mchango wake katika uchumi, ajira na fursa za uwekezaji, hususan kwa vijana.
Ameeleza kuwa ni muhimu kuimarisha mifumo ya udhibiti na usimamizi wa shughuli za madini kuanzia hatua ya ugunduzi, utoaji wa vibali, utafiti, uchimbaji, uchenjuaji na utunzaji wa mazingira hadi biashara, ulipaji wa kodi na tozo, ili Serikali na wadau wanufaike ipasavyo na rasilimali hizo.
Apendekeza Idara Mbili za Madini
Katika kuboresha utendaji wa sekta hiyo, Kapalata amependekeza Tume ya Madini kuwa na idara kuu mbili, ambazo ni Idara ya Rasilimali na Akiba ya Madini (Mineral Resources and Reserves Department) pamoja na Idara ya Maendeleo ya Madini (Minerals Development Department).
Amesema idara ya kwanza itajikita katika kutafuta, kuratibu, kulinda na kusimamia rasilimali na akiba ya madini, huku idara ya pili ikihusika na kubuni, kuratibu na kusimamia mikakati ya maendeleo ya sekta hiyo kwa mtazamo wa kibiashara.
Kwa mujibu wa Kapalata, mgawanyo huo utasaidia kuimarisha nguzo zilizopo na kuanzisha nguzo mpya za maendeleo zitakazozingatia aina mbalimbali za madini yanayopatikana nchini, kwa lengo la kuongeza tija na kuhakikisha sekta hiyo inakuwa endelevu kiuchumi.
Ataka Huduma za Madini Kufika Kata na Wilaya
Aidha, ameshauri Serikali kufanya tafiti yakinifu kuhusu muundo wa kiutendaji wa Wizara ya Madini na Tume ya Madini ili kuimarisha utoaji wa huduma kuanzia ngazi ya taifa, mkoa, wilaya hadi kata.
Amependekeza kuanzishwa kwa ofisi za maafisa madini wa wilaya na kata zitakazofanya kazi kwa kushirikiana na ofisi za maafisa madini wa mikoa, kwa kuzingatia majukumu na mahitaji ya maeneo husika.
Amesema hatua hiyo itarahisisha usimamizi, uratibu na uendelezaji wa shughuli za madini, ikiwemo utoaji wa vibali, ukusanyaji wa kodi na tozo pamoja na kushughulikia changamoto za wadau kwa wakati.
Ameongeza kuwa uimarishaji wa mfumo huo utasaidia kuiunganisha sekta ya madini na sekta nyingine za maendeleo, kama kilimo, mifugo, afya na maendeleo ya jamii, huku sera na mifumo ya usimamizi ikizingatia mabadiliko ya kijamii, kiteknolojia, kimazingira, kiusalama na kiuchumi.
Apendekeza Somo la Madini Shuleni
Katika hatua nyingine, Kapalata amependekeza kuanzishwa kwa mtaala wa elimu ya madini kuanzia shule za msingi na sekondari hadi vyuo vya kati na vya elimu ya juu ili kuongeza uelewa wa sekta hiyo na kuzalisha wataalamu wenye ujuzi unaohitajika.
Amesema elimu hiyo itasaidia kujenga msingi imara wa maarifa kuhusu rasilimali madini, fursa zake za kiuchumi na umuhimu wa matumizi endelevu ya rasilimali hizo.
Pia, ameshauri Serikali kuweka mazingira rafiki kwa wamiliki wa leseni za madini ili kupunguza gharama za utafiti, uendelezaji, uchimbaji na uchenjuaji wa madini.
Miongoni mwa mapendekezo yake ni kupunguza ukubwa wa juu wa eneo la leseni ya utafiti wa madini hadi kilometa za mraba 100 na kuongeza muda wa umiliki wa leseni hiyo hadi miaka 10, akieleza kuwa hatua hizo zinaweza kutoa muda wa kutosha kufanya utafiti na upembuzi yakinifu, kuongeza ushiriki wa wawekezaji na kupanua wigo wa walipa kodi na tozo.
Hata hivyo, amesisitiza umuhimu wa kufanya tafiti za kina kabla ya kufanya mabadiliko hayo ili kuhakikisha yanazingatia mahitaji ya sekta na maslahi ya taifa.
Azungumzia Migogoro ya Ardhi na Mikopo
Kapalata pia amependekeza kufanyika kwa tafiti za kina kuhusu uhusiano kati ya haki za umiliki wa ardhi na haki za umiliki wa madini, kwa kushirikisha wizara husika na wadau, ili kuweka utaratibu thabiti wa kisheria wa kutatua migogoro inayoweza kujitokeza kati ya wamiliki wa haki hizo.
Amesema utaratibu huo unapaswa kuzingatia haki na maslahi ya pande zote, huku ukiboresha mifumo iliyopo kwa ajili ya usimamizi endelevu wa sekta hiyo.
Vilevile, ameunga mkono pendekezo la kuanzishwa kwa bodi ya kisheria ya wataalamu wa jiolojia, itakayosaidia kuimarisha taaluma hiyo na ubora wa taarifa za kijiolojia zinazotumika katika shughuli za madini.
Kwa maelezo yake, taarifa sahihi za kijiolojia zinaweza kusaidia taasisi za kifedha kufanya tathmini bora za uwezekano na hatari za uwekezaji, hivyo kupanua fursa za wamiliki wa leseni za madini kupata mikopo kutoka taasisi za kibenki.
Amesisitiza kuwa kwa kuwa madini ni rasilimali zisizorejea kwa haraka, kutokana na kuchukua muda mrefu kuumbika kijiolojia, ni muhimu kuweka mifumo itakayohakikisha matumizi yake yana tija kwa taifa na vizazi vijavyo.
MAVUNDE APOKEA USHAURI
Akijibu hoja na maswali ya wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, Waziri wa Madini, Anthony Peter Mavunde, amempongeza Kapalata kwa ushauri wake na kueleza kuwa Wizara imeupokea kwa ajili ya kuufanyia kazi.
Mavunde amesema Wizara itaendelea kuzingatia maoni na mapendekezo yanayolenga kuboresha utendaji wake ili kuongeza tija katika usimamizi wa rasilimali madini na kuhakikisha taifa pamoja na wadau wa sekta hiyo wananufaika ipasavyo.
Kwa upande wake, Kapalata amemshukuru Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Subira Khamis Mgalu, Mbunge wa Bagamoyo, pamoja na Makamu Mwenyekiti, Simon Songe Lusengekile, Mbunge wa Busega, kwa uongozi wao.
Pia amempongeza Waziri Mavunde na timu ya Wizara ya Madini kwa juhudi na ubunifu katika kusimamia sekta hiyo, huku akisisitiza umuhimu wa kuendelea kuboresha mifumo na sera ili kuendana na mahitaji ya sasa na matarajio ya maendeleo ya taifa.









No comments:
Post a Comment