MHE. SALOME AKUTANA NA KAMPUNI ZA CHINA KUJADILI UWEKEZAJI KATIKA MAFUTA, GESI ASILIA NA NISHATI JADIDIFU - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Friday, October 23, 2026

MHE. SALOME AKUTANA NA KAMPUNI ZA CHINA KUJADILI UWEKEZAJI KATIKA MAFUTA, GESI ASILIA NA NISHATI JADIDIFU


Naibu Waziri wa Nishati, Mhe. Salome Makamba, amekutana na kufanya mazungumzo na viongozi wa kampuni mbili kutoka China kwa lengo la kujadili uwekezaji katika sekta ya nishati nchini, hususan katika shughuli za utafutaji wa mafuta na gesi asilia, ujenzi wa miundombinu ya gesi pamoja na miradi ya nishati jadidifu.

Katika kikao kilichofanyika Oktoba 23, 2026, katika Ofisi ndogo za Wizara ya Nishati, Dar es Salaam,
Mhe. Salome amefanya mazungumzo na Mkurugenzi wa Kampuni ya ChuanQing Drilling Company, Bw. Liu Chang Xu, yaliyolenga kujadili fursa za uwekezaji katika shughuli za utafutaji wa mafuta na gesi asilia, ujenzi wa miundombinu katika mkondo wa chini wa sekta ya petroli pamoja na miradi ya nishati jadidifu, hususan nishati ya jua na jotoardhi.

Pia, Mhe. Salome amezungumza na Mwenyekiti wa Kampuni ya Kwala Industries, Bw. Janson Huang, kuhusu hatua iliyofikiwa katika utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa bomba la kusafirisha gesi asilia kutoka Kinyerezi, Dar es Salaam, hadi Chalinze mkoani Pwani, unaoendelea kusimamiwa na Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC).

Mradi huo unatarajiwa kuwezesha upatikanaji wa gesi asilia kwa ajili ya matumizi ya viwanda katika eneo la Chalinze na maeneo jirani, hatua itakayochochea uwekezaji na kukuza shughuli za kiuchumi.

Vikao hivyo vimehudhuriwa pia na Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati (Mafuta na Gesi), Dkt. James Mataragio, pamoja na wataalam kutoka Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC).

No comments:

Post a Comment