Na Sixmund Begashe, Dodoma
WATAALAM wa Ufuatiliaji na Tathmini wa Wizara ya Maliasili na Utalii wametakiwa kuhakikisha kuwa wanafanya kazi zao kwa umakini na uadilifu mkubwa ili kuchechemua ufanisi wa kazi kwa watumishi wa Wizara hiyo ili kufikia malengo yaliyokusudiwa.
Wito huo umetolewa na Mkurugenzi wa Kitengo cha Ufuatiliaji na Tathmini Wizara ya Maliasili na Utalii Bi. Bure Nassibu alipokuwa akifunga Kikao Kazi cha wataalam hao Jijini Dodoma.
Bi. Nassibu amesema kuwa Serikali kupitia Wizara hiyo ina imani kubwa na wataalam hao katika kuhakikisha kuwa wanafuatilia kila hatua ya utekelezaji wa idara, vitengo na taasisi zake ili matokeo chanya yaonekane katika maisha ya wananchi.
Ameongeza kuwa kitengo hicho kitakuwa bega kwa bega na wataalam hao ili kuimarisha ufanisi wa utendaji kazi katika ngazi zote za Wizara hiyo.
"Mpango Mkakati wa Wizara yetu (2026/2027 – 2030/2031) umelenga kuhakikisha kuwa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 inafanikiwa, hivyo sisi kwa nafasi zetu tunatakiwa tufanye kazi kwa ufanisi mkubwa ili kuwezesha kufikiwa kwa malengo ya Serikali kwa manufaa ya Taifa kwa ujumla," alisisitiza Bi. Nassibu.
Naye Afisa Uhifadhi Mkuu - Mipango, Ufuatiliaji na Tathmini kutoka Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA), Bw. Emmanuel Igiha, pamoja na kupongeza jitihada za Wizara za kuhakikisha kuwa idara, vitengo na taasisi zilizo chini yake zinafuatilia na kutathmini sera, mipango, mikakati na miradi ya Wizara hiyo, amesema kikao hicho kimekuwa darasa tosha la kuimarisha uelewa wa wataalam hao.
Wizara ya Maliasili na Utalii kupitia Kitengo cha Ufuatiliaji na Tathmini imekuwa na utaratibu wa kuwakutanisha wataalam wake wa Ufuatiliaji na Tathmini kila Robo ya Mwaka ili kujadili na kuandaa taarifa ya ufuatiliaji wa utendaji kazi wa Wizara na taasisi zake.




No comments:
Post a Comment