
Mkutano wa Saba wa Tume ya Pamoja ya Kudumu ya Ushirikiano wa Ulinzi na Usalama kati ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Jamhuri ya Msumbiji (Joint Permanent Commission for Cooperation – JPCC) umefunguliwa rasmi tarehe 5 Oktoba 2026, jijini Dar es Salaam.
Mkutano huo umefunguliwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dkt. Faraji Kasidi Mnyepe, katika Ukumbi wa The Aga Khan Diamond Jubilee, Dar es Salaam.
Mkutano huo umehudhuriwa na Makatibu Wakuu, wawakilishi wa Wakuu wa Vyombo vya Ulinzi na Usalama, pamoja na wataalamu kutoka Tanzania na Msumbiji wanaohusika na masuala ya ulinzi na usalama.
Akifungua mkutano huo, Dkt. Mnyepe ameeleza kuwa ushirikiano kati ya Tanzania na Msumbiji katika nyanja ya diplomasia ya ulinzi na usalama una historia ndefu na umejengwa katika misingi ya ujirani mwema, urafiki na maslahi ya pamoja ya wananchi wa nchi hizo mbili.
Amesisitiza kuwa mkutano huo ni fursa muhimu kwa pande zote mbili kutathmini kwa pamoja masuala ya ulinzi na usalama, kubadilishana uzoefu na utaalamu, pamoja na kujadili maeneo ya kuimarisha ushirikiano wa nchi hizo mbili.
Aidha, Dkt. Mnyepe amewataka wajumbe na wataalamu kutumia ipasavyo fursa hiyo kwa kujadili kwa kina na kwa mtazamo wa pamoja masuala yaliyo kwenye ajenda ya mkutano, ili kufikia maazimio yenye tija yatakayotekelezwa kwa ufanisi na kuleta manufaa kwa Tanzania na Msumbiji.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Wizara ya Ulinzi ya Msumbiji, Bw. Casimiro Augusto Mueio, ameishukuru Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa mapokezi mazuri na ukarimu ulioonyeshwa kwa ujumbe wa Msumbiji tangu ulipowasili nchini.
Bw. Mueio ameeleza matumaini yake kuwa majadiliano yatakayofanyika katika Mkutano huo wa Saba yatawezesha pande zote mbili kupata suluhisho la pamoja kwa masuala mbalimbali ya ulinzi na usalama, na hivyo kuendelea kuimarisha ushirikiano wa kimkakati kati ya Tanzania na Msumbiji kwa manufaa ya nchi hizo mbili na ustawi wa wananchi wake.
Tanzania na Msumbiji zina historia ya muda mrefu ya uhusiano wa kidiplomasia, ambao ulijengeka kwa nguvu katika kipindi cha harakati za ukombozi wa nchi za Kusini mwa Afrika. Tanzania ilitoa mchango mkubwa katika harakati hizo, ikiwemo kuunga mkono mapambano ya ukombozi wa Msumbiji na nchi nyingine za Kusini mwa Afrika.
Msingi huo wa kihistoria umeendelea kuwa nguzo muhimu katika kuimarisha uhusiano na ushirikiano kati ya Tanzania na Msumbiji katika maeneo mbalimbali, hususan ulinzi na usalama, kwa lengo la kulinda amani, utulivu na maslahi ya pamoja ya nchi hizo mbili.
Mkutano huo wa Saba wa Tume ya Pamoja ya Kudumu ya Ushirikiano wa Ulinzi na Usalama unalenga, miongoni mwa mambo mengine, kupitia utekelezaji wa maeneo ya ushirikiano yaliyokubaliwa na pande hizo mbili, kubaini maeneo mapya ya ushirikiano, pamoja na kuweka mikakati ya pamoja ya kukabiliana na changamoto za ulinzi na usalama zinazozikabili nchi hizo na ukanda kwa ujumla.






No comments:
Post a Comment