
Na Erick Nenda, OKULY BLOG, DODOMA
Serikali imeeleza kuwa inaendelea kuweka mazingira rafiki kwa waendesha bodaboda nchini ili kuwawezesha kuongeza kipato, kuimarisha shughuli zao za kiuchumi na kutumia fursa zilizopo kuchangia maendeleo ya Taifa.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Eliakim Chacha Maswi, amesema hayo Oktoba 19, 2026, jijini Dodoma, wakati wa kikao na viongozi na wawakilishi wa waendesha bodaboda kutoka mikoa ya Dodoma, Dar es Salaam, Morogoro, Tanga, Singida, Arusha na Njombe.
Kikao hicho kililenga kujadili mikakati ya kuwawezesha waendesha bodaboda kiuchumi, kutambua changamoto zinazowakabili na kuweka njia za kuboresha mazingira yao ya kazi.
Maswi amesema waendesha bodaboda ni sehemu muhimu ya uchumi wa Taifa kutokana na mchango wao katika kutoa huduma za usafiri, kusafirisha bidhaa, kujiajiri na kutengeneza fursa za ajira, hususan kwa vijana.
“Ninachoomba kwenu ni kuiona sekta ya usafiri wa bodaboda inakuwa na hadhi, madereva wenye weledi na uwezo wa kujiongezea kipato, kwa manufaa yao binafsi na Taifa kwa ujumla,” amesema Maswi.
Amesema Serikali imeanzisha programu tumizi ya Jamii Wezesha, inayolenga kurahisisha upatikanaji wa taarifa na fursa za uwezeshaji wa kiuchumi kwa wafanyabiashara wadogo nchini, wakiwemo waendesha bodaboda.
Kwa mujibu wa Maswi, matumizi ya teknolojia kupitia programu hiyo yanalenga kurahisisha utambuzi na usajili wa wafanyabiashara wadogo ili waweze kupata taarifa kuhusu fursa mbalimbali za kiuchumi na kunufaika nazo.
Kwa upande wake, Kiongozi wa Chama cha Waendesha Pikipiki Tanzania (CHAWAPITA), Daudi Laurian, amesema bado kuna umuhimu wa jamii kubadili mitazamo hasi dhidi ya waendesha bodaboda na kutambua mchango wao katika kukuza uchumi wa familia na Taifa.
Laurian amesisitiza umuhimu wa kuwapatia madereva elimu ya uwekezaji na usimamizi wa fedha ili waweze kupanga matumizi yao, kutofautisha mahitaji muhimu na yasiyo ya lazima, kuweka akiba na kuanzisha miradi mingine ya kuwaongezea kipato.
Amebainisha pia kuwa changamoto zinazohusiana na mifumo ya ulipaji wa mapato zinahitaji kupewa kipaumbele na kutafutiwa ufumbuzi ili kurahisisha utekelezaji wa majukumu ya waendesha bodaboda.
Kikao hicho ni sehemu ya juhudi za kuimarisha ushirikiano kati ya Serikali na viongozi wa waendesha bodaboda, kwa lengo la kutafuta ufumbuzi wa changamoto zao, kupanua fursa za kiuchumi na kuongeza mchango wa sekta hiyo katika maendeleo ya Taifa.







No comments:
Post a Comment