
Na Shaban Juma, WAF – Dodoma
Serikali imeeleza kuwa inaendelea kuimarisha mikakati ya kukabiliana na utapiamlo nchini kwa kuweka mkazo katika huduma za lishe kwa mama na mtoto, urutubishaji wa vyakula, kuongeza wataalamu wa lishe na kuimarisha elimu kwa wananchi ili kulinda afya na maendeleo ya rasilimali watu.
Hayo yamesemwa leo oktoba 15,2026 na Naibu Waziri wa Afya, Dkt. Florence Samizi Kwa niaba ya Waziri wa Afya Mhe.Mohamed Mchengerwa wakati wa kuwasilisha taarifa ya Wizara ya Afya kuhusu mpango na mkakati wa kuimarisha lishe nchini mbele ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Afya na Masuala ya UKIMWI.
Dkt. Samizi amesema kuwa lishe bora ni msingi wa afya njema, ukuaji wa watoto na maendeleo ya Taifa, akieleza kuwa Serikali inaendelea kutekeleza afua mbalimbali zinazolenga kuzuia na kudhibiti aina zote za utapiamlo, ikiwemo udumavu, ukondefu, upungufu wa vitamini na madini, pamoja na uzito uliozidi na kiribatumbo.
Amesema kuwa Tanzania imepiga hatua katika kupunguza udumavu kwa watoto walio chini ya miaka mitano kutoka asilimia 34 mwaka 2015/16 hadi asilimia 30 mwaka 2022. Aidha, kiwango cha ukondefu kilipungua hadi asilimia tatu mwaka 2022, ingawa bado kuna changamoto zinazohitaji juhudi zaidi, hususan katika maeneo yenye viwango vya juu vya utapiamlo.
Ameongeza kuwa Serikali chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan inaendelea kuimarisha afua za lishe katika siku 1,000 za mwanzo za maisha ya mtoto, kupitia kuhamasisha unyonyeshaji wa maziwa ya mama pekee kwa miezi sita ya mwanzo, ulishaji sahihi wa vyakula vya nyongeza, ufuatiliaji wa ukuaji wa mtoto na utoaji wa virutubishi muhimu.







No comments:
Post a Comment