
NA MWANDISHI WETU - SONGWE
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Deogratius Ndejembi, amewataka Mawaziri na watendaji wa Serikali kuhakikisha miradi ya maendeleo inakamilika kwa wakati na kuleta matokeo yanayogusa maisha ya wananchi, akisisitiza kuwa Watanzania wanahitaji huduma za uhakika badala ya ahadi zisizotekelezwa.
Akizungumza na wananchi wa Tunduma mkoani Songwe wakati wa ziara yake ya kikazi, Mhe. Ndejembi ameagiza kuharakishwa kwa utekelezaji wa mradi mkubwa wa maji wa Tunduma, ambao Rais tayari ametoa malipo ya awali, huku akiitaka TANESCO kuhakikisha Kituo cha Kupoza na Kusambaza Umeme cha Nkangamo kinawashwa ifikapo Desemba 2026.
Aidha, amemwelekeza Waziri wa Ujenzi, Mhe. Masanja Kadogosa, kumsimamia mkandarasi ili kuhakikisha ujenzi wa barabara katika eneo hilo unakamilika ifikapo Oktoba 31, 2026, kama ilivyoahidiwa.
Makamu wa Rais amesisitiza kuwa maendeleo hayana itikadi za kisiasa wala mipaka ya maeneo, hivyo viongozi wanapaswa kutanguliza maslahi ya wananchi kwa kuhakikisha huduma muhimu zinapatikana kwa wakati.
Awali, Mhe. Ndejembi alikagua ujenzi wa Kituo cha Umeme cha Nkangamo, wilayani Momba, unaogharimu shilingi bilioni 285.7, ambapo utekelezaji wake umefikia asilimia 83.13. Mradi huo unatarajiwa kuimarisha upatikanaji wa umeme mkoani Songwe, kuchochea uzalishaji viwandani na kufungua fursa za biashara ya umeme kati ya Tanzania na nchi za Kusini mwa Afrika.





No comments:
Post a Comment