
Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar (Mb) amesema Tanzania inaunga mkono mkakati maalum wa Benki ya Dunia wa kuzisaidia nchi wanachama kuweka mipango ya maendeleo na miradi itakayochochea upatikanaji wa ajira hususan kwa vijana na kukuza sekta binafsi ili kuharakisha maendeleo ya kiuchumi.
Mhe. Balozi Omar (Mb), amesema hayo jijini Bangkok nchini Thailand, wakati wa Mkutano wa Kundi la Kwanza la nchi za Kanda ya Afrika, wanachama wa Benki ya Dunia, uliofanyika kando ya Mikutano ya Mwaka ya Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) na Benki ya Dunia, inayoendelea nchini humo.
Amesema ajira ni suala la kipaumbele kwa Tanzania na Afrika kwa ujumla kutokana na kuwepo kwa idadi kubwa ya watu, ambayo sehemu kubwa inaundwa na watoto na vijana wanaohitaji fursa za elimu, ujuzi na ajira ili kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya kiuchumi.
Alieleza kuwa Serikali itaendelea kuwekeza katika elimu na ukuzaji wa ujuzi ili kuwawezesha vijana kupata ajira na kujiajiri, huku akisisitiza umuhimu wa kuongeza fursa za ajira kupitia sekta zenye uwezo mkubwa wa kuzalisha ajira nchini zikiwemo Sekta za kilimo, uchimbaji na uchakataji wa madini pamoja na utalii.
Mhe. Balozi Omar amesema lazima kuongeza juhudi si tu katika uzalishaji wa mazao pekee, bali katika kuongeza thamani kupitia usindikaji na uanzishaji wa viwanda vinavyotumia malighafi za ndani, hatua itakayo ongeza fursa za ajira, kukuza biashara na kuimarisha mchango wa sekta hiyo katika uchumi.
Vilevile, alisisitiza umuhimu wa kuhakikisha kuwa miradi mikubwa ya maendeleo inayotekelezwa nchini inatoa fursa kwa sekta binafsi, hususan wawekezaji wa ndani, kushiriki katika utekelezaji wake na kunufaika na fursa za kiuchumi zinazotokana na uwepo wa miradi hiyo.
Akitoa taarifa ya utekelezaji wa majukumu ya Benki ya Dunia, Mkurugenzi Mtendaji wa Kundi la Kwanza la Afrika la nchi wanachama wa Taasisi hiyo, Dkt. Zarau Wendeline Kibwe, amezihimiza nchi hizo kuhakikisha kuwa suala la ajira linapewa kipaumbele katika sekta zote za maendeleo.
Wakati huo huo, Magavana wa Benki ya Dunia wa Kundi la Kwanza la Afrika wametumia mkutano huo kumuaga rasmi Mkurugenzi Mtendaji wa Kundi hilo, Dkt. Zarau Kibwe ambaye ni Mtanzania, baada ya kumaliza muda wake na kummwagia sifa kemkem kwa utendaji kazi wake uliotukuka katika kipindi cha miaka miwili aliyoitumia nafasi hiyo, kuanzia mwaka 2024 hadi Oktoba 2026.
Mhe. Balozi Omar amesema Tanzania inajisikia Fahari kuona kuwa Magavana wote kwa umoja wao wameridhika na umahiri wa Dkt. Kibwe katika uongozi na kufanikisha nchi hizo kunufaika na misaada ya fedha na kiufundi, mikopo nafuu na na kuiweka Tanzania katika ramani ya dunia kwa kushawishi mikutano ya kimataifa ya Taasisi hiyo kufanyika nchini Tanzania kwa mafanikio makubwa.
Kwa upande wake Dkt. Kibwe, amemshukuru Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kumwamini na kumteua kushika nyadhifa mbalimbali katika Taasisi hiyo kubwa ya fedha duniani na kwamba uzoefu alioupata utamsadia kutoa mchango wake kwa Taifa.
Amesema kuwa miongoni mwa masuala anayojivunia katika kipindi chake cha utumishi cha miaka miwili jijini Washington D.C ni pamoja na kuweka mikakati ya Benki kuongeza kiwango cha fedha kwa nchi za Kundi lake lenye nchi 22 kupata jumla ya dola za Marekani bilioni 29 kupitia taasisi mbalimbali za Kundi la Benki hiyo.
Dkt. Kibwe amesema tangu aingie katika Bodi ya Wakurugenzi ya Benki ya Dunia, Tanzania, imefanikiwa kuongeza kiwango chake cha fedha kutoka dola za Marekani bilioni 4 hadi kufikia dola bilioni 9 zilizoelekezwa kwenye miradi ya maendeleo ya kimkakati huku kiwango cha fedha zilizoelekezwa kusaidia sekta binafsi kimeongeza kutoka dola milioni 200 hadi dola za Marekani milioni 800.
Jalada la miradi ya sekta ya umma inayoungwa mkono na Benki hiyo limeongezeka kutoka takribani dola za Marekani bilioni 4 alipokuwa akijiunga na Bodi ya Benki ya Dunia hadi kufikia takribani dola za Marekani bilioni 9, huku ufadhili kwa sekta binafsi ukiongezeka kutoka takribani dola milioni 200 hadi dola milioni 800.





No comments:
Post a Comment