Na Saidi Saidi, WMJJWM
Serikali imetoa wito kwa jamii kuwekeza kwa mtoto wa kike kwa kuhakikisha analindwa, anapata elimu na analelewa katika mazingira salama.
Wito huo umetolewa na Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima, leo Oktoba 07, 2026, jijini Dar es Salaam, wakati akizungumza na waandishi wa habari kuelekea Maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Mtoto wa Kike yanayofanyika Oktoba 11, 2026, yenye kaulimbiu “Wekeza kwa Mtoto wa Kike: Tokomeza Ndoa za Utotoni.”
Dkt. Gwajima amewaeleza wazazi na walezi kuhakikisha watoto wa kike wanapata malezi bora, ikiwa ni pamoja na kuchukua hatua za kutokomeza ndoa za utotoni na ukatili dhidi ya watoto.
Aidha, amewataka watoto wa kike, hususan wanafunzi, kusoma kwa bidii, kuweka malengo makubwa, kujiamini, kuendeleza vipaji na ujuzi wao pamoja na kutumia teknolojia na mitandao ya kijamii kwa usalama na kwa manufaa.
Amewahimiza pia, kutokubali ndoa za utotoni, ukatili, unyanyasaji au shinikizo la mtu mwingine kukatiza elimu na ndoto zao, na kutoa taarifa kwa mzazi, mlezi, mwalimu, kiongozi wa jamii au chombo husika wanapokutana na changamoto.
Wakati huo huo, Waziri Gwajima amewasihi waandishi wa habari, kuendelea kuelimisha jamii na kupinga mila, desturi na mitazamo inayoweza kumdhalilisha au kumzuia mtoto wa kike kufikia uwezo wake, huku vyombo vya habari vikitumia nafasi yao kutoa elimu kuhusu haki za mtoto, madhara ya ndoa za utotoni na ukatili kwa kuzingatia utu, usalama na faragha ya watoto.
Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu wakili Amon Mpanju, akimwakilisha Katibu Mkuu wa Wizara, Eliakim Maswi, amesema Serikali itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali wa elimu, familia, jamii na taasisi zinazohusika kuhakikisha watoto wa kike wanapata fursa ya kuendelea na elimu, wanalindwa dhidi ya ndoa za utotoni, ukatili, unyanyasaji na ubaguzi.
Vile, kuhakikisha wanapata mazingira salama ya kukua na kutimiza ndoto zao. Amesema ushirikiano huo ni muhimu katika kuimarisha hatua za kuzuia ukatili, kutoa taarifa mapema na kuhakikisha watoto wanaopitia changamoto wanapata huduma na ulinzi stahiki.








No comments:
Post a Comment