
Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Fedha, Bw. Elijah Mwandumbya akifungua kikao cha ngazi ya wataalam cha Mafungu yote yanayokusanya mapato yasiyo ya kodi kilichofanyika jijini Dodoma katika ukumbi wa Kambarage, Treasury Square.

Mkurugenzi wa Idara ya Usimamizi wa Mifumo ya Fedha na Tehama, Wizara ya Fedha, Dkt. John Sausi, akitoa maelezo mafupi wakati wa kikao cha ngazi ya wataalam cha mafungu yote yanayokusanya mapato yasiyo ya kodi kilichofanyika jijini Dodoma katika ukumbi wa Kambarage, Treasury Square.

Mkurugenzi wa Idara ya Mipango, Wizara ya Fedha, Bw. Amoury Amoury, akiteta jambo na Afisa Usimamizi wa Fedha Mkuu, Idara ya Uchambuzi wa Sera Bi. Emerensiana Nyanda, wakati wa kikao cha ngazi ya wataalam cha mafungu yote yanayokusanya mapato yasiyo ya kodi kilichofanyika jijini Dodoma katika ukumbi wa Kambarage, Treasury Square.

Sekretarieti wakichukua maoni kutoka kwa wachangiaji wa maoni wakati wa kikao cha ngazi ya wataalam cha mafungu yote yanayokusanya mapato yasiyo ya kodi kilichofanyika jijini Dodoma katika ukumbi wa Kambarage, Treasury Square.

Baadhi ya wajumbe wa kikao cha ngazi ya wataalam cha mafungu yote yanayokusanya mapato yasiyo ya kodi wakifuatilia mawasilisho mbalimbali wakati wa kikao hicho kilichofanyika jijini Dodoma katika ukumbi wa Kambarage, Treasury Square.

Afisa Usimamizi wa Fedha, Idara ya Uchambuzi wa Sera, Wizara ya Fedha, Bw. David Massawe, akifanya wasilisho kuhusu taarifa ya utekelezaji wa mkakati wa mud awa kati wa ukusanyaji wa mapato wakati wa kikao cha ngazi ya wataalam cha mafungu yote yanayokusanya mapato yasiyo ya kodi kilichofanyika jijini Dodoma katika ukumbi wa Kambarage, Treasury Square.

Meneja wa Mfuko wa Maendeleo ya Kilimo, Wizara ya Kilimo, Bi. Maria Mtui, akifanya wasilisho kuhusu ukusanyaji wa mapato yasiyokuwa ya kikodi katika Sekta ya Kilimo, wakati wa kikao cha ngazi ya wataalam cha mafungu yote yanayokusanya mapato yasiyo ya kodi kilichofanyika jijini Dodoma katika ukumbi wa Kambarage, Treasury Square.

Mkurugenzi Msaidizi, Ofisi ya Msajili wa Hazina Bw. Joseph Mwaisemba, akifanya wasilisho kuhusu taarifa ya makusanyo ya mapato yasiyo ya kodi wakati wa kikao cha ngazi ya wataalam cha mafungu yote yanayokusanya mapato yasiyo ya kodi kilichofanyika jijini Dodoma katika ukumbi wa Kambarage, Treasury Square.

Mhasibu Mkuu, Wizara ya Mifugo na Uvuvi Bw. Richard Masini, akifanya wasilisho kuhusu taarifa ya makusanyo ya mapato yasiyo ya kodi wakati wa kikao cha ngazi ya wataalam cha mafungu yote yanayokusanya mapato yasiyo ya kodi kilichofanyika jijini Dodoma katika ukumbi wa Kambarage, Treasury Square.
(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, WF, Dodoma)
Farida Radhaman na Josephine Majura, WF, Dodoma
Serikali imeziagiza taasisi zote zinazohusika na ukusanyaji wa mapato yasiyo ya kodi kuimarisha mifumo ya ukusanyaji, usimamizi na ufuatiliaji wa fedha ili kuhakikisha kila shilingi inayostahili kukusanywa inaingia katika mifumo rasmi ya Serikali na kusaidia kugharamia huduma za jamii pamoja na miradi ya maendeleo.
Wito huo umetolewa jijini Dodoma na Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Fedha, Bw. Elijah Mwandumbya, wakati akifungua kikao cha wataalum cha mafungu yanayohusika na ukusanyaji wa mapato yasiyo ya kodi, kwa lengo la kupitia taarifa za makusanyo, kujadili changamoto na kuandaa mapendekezo yatakayosaidia kuboresha usimamizi wa mapato ya Serikali.
Bw. Mandumbya alisisitiza kuwa kuongeza viwango vya tozo au kubaini vyanzo vipya vya mapato pekee hakutoshi bila kuimarisha mifumo ya ukusanyaji na kudhibiti mianya ya upotevu wa fedha za umma.
“Ni muhimu kuhakikisha kila shilingi inayostahili kukusanywa na Serikali inaingia katika mifumo rasmi. Tunapaswa kuimarisha usimamizi na ufuatiliaji wa mapato ili kuzuia upotevu wa fedha ambazo ni muhimu katika utekelezaji wa mipango ya Serikali na utoaji wa huduma kwa wananchi,” alisisitiza Bw. Mwandumbya.
Alisema kuwa juhudi za kuongeza mapato zinapaswa kuzingatia hali halisi ya uchumi na kulinda mazingira yanayowawezesha wananchi kufanya shughuli halali za kiuchumi.
Aliongeza kuwa ukusanyaji wa mapato yasiyo ya kodi ni jukumu la pamoja linalohitaji ushiriki wa taasisi zote katika hatua za upangaji wa makadirio, utekelezaji, ufuatiliaji na tathmini huku akiwasihi kutumia kikao hicho kuweka maazimio yenye mikakati inayotekelezeka, majukumu yaliyo wazi na utaratibu madhubuti wa kufuatilia matokeo.
“Lengo letu si kuongeza mapato pekee, bali pia kuhakikisha hakuna fedha zinazopaswa kuingia Serikalini zinazopotea kutokana na udhaifu wa mifumo au usimamizi usioridhisha. Kila taasisi inapaswa kutekeleza wajibu wake na kuhakikisha maazimio yanayokubaliwa yanafuatiliwa hadi kuleta matokeo,” alieleza Bw. Mwandumbya.
Alisema Takwimu za makusanyo ya mwaka wa fedha 2025/26 zinaonesha kuwa mchango wa mapato yasiyo ya kodi unatofautiana kwa kiasi kikubwa kati ya taasisi za Serikali, huku baadhi zikichangia sehemu kubwa ya mapato na nyingine zikiwa na mchango mdogo.
Bw. Mwandumbya alisema takwimu hizo zinaonesha umuhimu wa taasisi zenye mchango mdogo kupitia upya mikakati yao na kujifunza kutoka kwa taasisi zinazofanya vizuri.
“Bado kuna fursa nyingi za mapato ambazo hazijafikiwa kikamilifu. Ni muhimu kwa kila taasisi kubaini fursa hizo na kuimarisha usimamizi ili kuongeza mchango wake katika mapato ya Serikali,” alisisitiza Bw. Mwandumbya.
Bw. Mwandumbya alisema pamoja na changamoto hizo, mapato yasiyo ya kodi yameendelea kuonesha ongezeko. Katika kipindi cha Julai hadi Agosti cha mwaka wa fedha 2026/27, Serikali ilikusanya shilingi trilioni 1.06 sawa na ufanisi wa asilimia 114.7 ya lengo la kipindi hicho.
Alisema makusanyo hayo yanaonesha ukuaji wa asilimia 34.4 ikilinganishwa na kipindi kama hicho mwaka 2025, na kubainisha kuwa katika mwaka wa fedha 2025/26, Serikali ilikusanya shilingi trilioni 4.3175 kati ya lengo la shilingi trilioni 4.682, sawa na ufanisi wa asilimia 92.2.
Kwa upande wake, Mkurungenzi wa Idara ya Mipango wa Wizara ya Fedha, Bw. Amoury Amoury ambaye alitoa maelezo ya awali kuhusu kikao hicho kwa niaba ya Kamishna wa Idara ya Uchambuzi wa Sera, Wizara ya Fedha, Dkt. Remidius Ruhinduka, alisema katika kikao hicho, washiriki watapata fursa ya kutathmini utekelezaji wa maazimio ya kikao kilichopita pamoja na kujadili mwenendo wa ukusanyaji wa mapato yasiyo ya kodi na usajili wa vyanzo vya mapato.
Alisema kikao hicho kililenga kupata mapendekezo ya kitaalamu yanayosisitiza umuhimu wa kuimarisha usimamizi wa vyanzo vilivyopo, kubaini fursa mpya za mapato na kuongeza uelewa wa wadau kuhusu taratibu za usajili, ili kuboresha usimamizi na ukusanyaji wa mapato yasiyo ya kodi kwa kusaidia kupanua wigo wa ukusanyaji wa mapato na kuongeza mchango wa mapato yasiyo ya kodi katika kugharamia shughuli za Serikali na miradi ya maendeleo.
Naye Mkurugenzi wa Mifumo ya Usimamizi wa Fedha na Huduma za Tehama, Dkt. John Sausi alielezea hatua mbalimballi zinazofanywa na Serikali kupitia Wizara ya Fedha katika kuboresha matumizi ya mifumo ya kidijitali, ikiwemo mfumo wa Control Number, ili kuongeza ufanisi na kurahisisha malipo ya huduma za Serikali.
Dkt. Sausi alisema kuwa baadhi ya changamoto zinazoathiri ufanisi wa mifumo hiyo ni pamoja na kuchelewa kwa taasisi kufanya upatanisho wa miamala (reconciliation) na hitilafu za kiufundi zinazoweza kujitokeza katika mifumo ya benki.
Alisema taasisi za Serikali zimetakiwa kufanya uhakiki wa miamala na taarifa za akaunti zao kwa wakati, huku ushirikiano kati ya Serikali, benki na wadau wa mifumo ukiendelea kuimarishwa ili kuhakikisha mapato yote yanayostahili yanakusanywa na kurekodiwa ipasavyo.
Kikao hicho ni sehemu ya maandalizi ya kikao kazi cha Maafisa Masuuli wa mafungu yote yanayokusanya mapato yasiyo ya kodi ili kwa pamoja kufanya tathmini ya ukusanyaji wa mapato kwa mwaka wa fedha 2025/26 na mikakati ilyowekwa kwa kila Fungu ili kufikia malengo ya mapato ya mwaka 2026/27 kinachotarajia kufanyika hivi karibuni.

No comments:
Post a Comment