USALAMA WA MABWAWA NI USALAMA WA TAIFA - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Thursday, October 22, 2026

USALAMA WA MABWAWA NI USALAMA WA TAIFA



Na Mwandishi Wetu - Mwanza


Usalama wa mabwawa ni moja ya nguzo muhimu ya kuhakikisha usalama imara wa Taifa wakati wote.

Dkt. Herman Nyigo kutoka Chuo cha Taifa cha Ulinzi (NDC), amesema usalama wa mabwawa ni sehemu muhimu ya usalama wa Taifa kwasababu ya mchango wake katika kufua nishati ya umeme, upatikanaji wa maji na ustawi wa wananchi.

Akizungumza Oktoba 22, 2026 katika mkutano wa mwaka wa Usalama wa Mabwawa Jijini Mwanza, amesisitiza umuhimu wa kulinda miundombinu hiyo dhidi ya hatari zinazoweza kuathiri huduma muhimu kwa wananchi.

Ametoa mfano wa Bwawa la Mwalimu Nyerere, Dkt. Nyigo ameeleza kuwa usalama wake unapewa kipaumbele kwa kuwa linachangia uzalishaji wa nishati ya umeme unaohudumia maeneo mbalimbali nchini. Amesisitiza kuwa hitilafu au athari yoyote kubwa katika miundombinu hiyo inaweza kuathiri shughuli za kiuchumi, kijamii na huduma muhimu kwa wananchi.

Amegusia umuhimu wa kuhakikisha usalama wa bwawa la Kidunda linalotarajiwa kuongeza upatikanaji wa maji kwa wakazi wa Dar es Salaam, Morogoro na Pwani. Ameeleza kuwa kulinda miundombinu hiyo ni muhimu katika kuhakikisha huduma ya uhakika ya maji , na maandalizi ya usalama yakizingatia vihatarishi vinavyoweza kujitokeza wakati wa ujenzi na uendeshaji wake.

Katika mkutano huo, washiriki wamejadili mikakati ya kuzuia majanga ya mafuriko, kuimarisha usalama na uimara wa mabwawa ya udongo na mawe katika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, pamoja na matumizi ya mifumo ya kiotomatiki kufuatilia hali ya mabwawa na kutoa tahadhari za mapema. Mada hizo zimejikita katika kuboresha utambuzi wa vihatarishi na kuongeza uwezo wa kukabiliana na dharura.

Aidha, wataalamu wamejadili teknolojia za ufuatiliaji wa usalama na utoaji wa tahadhari za mapema kwa mabwawa, ikiwemo mfumo wa utabiri wa hali mbalimbali za hatari, pamoja na umuhimu wa kutumia vipimo na uchambuzi wa kitaalamu kuelewa tabia na hali ya miundombinu hiyo. Hatua hizo ni muhimu katika kusaidia maamuzi ya kiufundi na kuzuia ajali zinazoweza kusababisha madhara makubwa.





No comments:

Post a Comment