WATU ZAIDI YA 28 WAFARIKI AJALI YA BASI NA LORI MOROGORO - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Friday, October 9, 2026

WATU ZAIDI YA 28 WAFARIKI AJALI YA BASI NA LORI MOROGORO



Watu zaidi ya 28 wamefariki dunia katika ajali iliyohusisha basi la abiria lililokuwa likitoka Dar es Salaam kuelekea Mbeya na lori aina ya Scania lililokuwa limebeba miti aina ya milunda, baada ya magari hayo kugongana uso kwa uso na basi kushika moto.

Ajali hiyo imetokea usiku wa kuamkia leo, Ijumaa, Oktoba 9, 2026, katika eneo la Mkambarani, barabara ya Morogoro–Dar es Salaam.

Kwa mujibu wa Kaimu Kamanda wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Morogoro, Joseph Mwasabeja, kati ya watu 29 waliofariki, 28 walikuwa abiria wa basi hilo huku mmoja akiwa kwenye lori.

Mwasabeja amesema baada ya magari hayo kugongana uso kwa uso, basi lilishika moto na kuteketea kabisa.

Akieleza chanzo cha ajali hiyo, amesema dereva wa lori, ambaye jina lake bado halijafahamika, alikuwa akitoka Iringa kuelekea Dar es Salaam na alitaka kuyapita magari mengine bila kuchukua tahadhari, hali iliyosababisha ajali hiyo.

Amesema idadi ya majeruhi bado haijafahamika rasmi, kwa kuwa baadhi walipelekwa hospitalini huku ilikosekana taarifa sahihi kuhusu mahali walipopelekwa wengine.

“Idadi ya majeruhi waliokuwa kwenye basi bado haijafahamika, kwani wengine walipelekwa hospitalini huku wengine haikujulikana rasmi walikoenda,” amesema Mwasabeja.

Kwa upande wake, Ofisa wa Kitengo cha Habari na Uhusiano wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Morogoro, Scholastica Ndunga, amesema taarifa rasmi kuhusu idadi ya waliofariki na majeruhi waliopokelewa hospitalini hapo itatolewa baadaye.




No comments:

Post a Comment