BBT KUPELEKA VIJANA 2,437 MASHAMBANI KATIKA HALMASHAURI 18 - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Friday, October 9, 2026

BBT KUPELEKA VIJANA 2,437 MASHAMBANI KATIKA HALMASHAURI 18



Na Boniphace John Epimack – DODOMA


Waziri wa Kilimo, Daniel Chongolo, amewataka vijana 2,437 waliochaguliwa kujiunga na mafunzo ya kilimo biashara kupitia Mradi wa Jenga Kesho Bora (BBT) kuripoti kwa wakati katika vituo walivyopangiwa na kuzingatia masharti yote ya mafunzo hayo.

Chongolo ametoa wito huo Oktoba 8, 2026, jijini Dodoma, akieleza kuwa vijana hao wanapaswa kuripoti katika vituo vyao kati ya Oktoba 24 na 25, mwaka huu, kabla ya kuanza mafunzo yatakayowaandaa kushiriki katika uzalishaji wa mazao ya kilimo.

Amesema Serikali itagharamia mafunzo, malazi na posho ya kujikimu ya kila mwezi kwa vijana hao katika kipindi chote cha mafunzo ya uatamizi.

“Kabla ya kuanza uzalishaji katika mashamba yaliyotengwa, vijana hao watapatiwa mafunzo ya kilimo biashara katika vituo atamizi vilivyoandaliwa kwa kipindi cha miezi miwili,” amesema Chongolo.

Ametaja mashamba yaliyotengwa kwa ajili ya mradi huo kuwa katika Halmashauri za Kaliua (Limbula), Muleba (Makongora), Kisarawe (Palaka), Bahi (Ikumburu), Misenyi (Kyakakera), Chemba (Gwandi), Njombe Mjini (Lwangu), Mpanda (Mwamkulu), Musoma DC (Bugwema), Kibaha (Mkino), Chunya (Lwalaje) na Ikungi.

Ameongeza kuwa katika mwaka wa fedha 2026/2027, mafunzo hayo yataendeshwa kwa awamu mbili, ambapo awamu ya kwanza itahusisha vijana 1,218 na awamu ya pili vijana 1,219, ambao kwa pamoja watafikia 2,437.

Kwa upande wake, Mratibu wa Mradi wa BBT Project One, Vumilia Zikankuba, amesema programu hiyo iko wazi kwa Watanzania wote, huku akieleza kuwa Serikali imebadilisha utaratibu wa ugawaji wa mashamba ili kurahisisha upatikanaji wa fursa kwa vijana.

Zikankuba amesema awali Serikali ndiyo iliyokuwa na jukumu la kutenga mashamba, lakini sasa jukumu hilo limekabidhiwa kwa Halmashauri, ambazo pia zinahusika na kuwadahili vijana kutoka maeneo yao.

“Miongoni mwa sababu za msingi za kubadilisha utaratibu huo ni kuwarahisishia vijana kufika mashambani kwa urahisi. Hapo awali vijana walipangwa maeneo ya mbali na iliwalazimu kusafiri umbali mrefu,” amesema.

Amefafanua kuwa utaratibu huo mpya unalenga kuwapa vijana fursa ya kushiriki katika mafunzo na shughuli za kilimo biashara kwa urahisi zaidi, kwa kuzingatia maeneo wanayoishi na mashamba yaliyotengwa na Halmashauri zao.







No comments:

Post a Comment