
Na Mwandishi Wetu, Mbeya
WIZARA na Taasisi za Umma zimetakiwa kuimarisha mikakati ya kudhibiti VVU, UKIMWI na Magonjwa Sugu Yasiyoambukiza (MSY), pamoja na kuweka mazingira rafiki yanayolinda afya ya akili ya watumishi ili kuongeza tija na kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi.
Wito huo umetolewa Oktoba 19, 2026, na Mwakilishi wa Katibu Mkuu wa Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, ambaye pia ni Mkurugenzi Msaidizi wa Sehemu ya Ufuatiliaji wa Sera, Bw. Olgatho Mwinuka, wakati akifungua kikao cha robo ya kwanza ya mwaka wa fedha 2026/2027 cha Kamati ya Kitaifa ya Kudhibiti VVU, UKIMWI na Magonjwa Sugu Yasiyoambukiza, kilichofanyika katika ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mbeya.
Akizungumza katika kikao hicho kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Ofisi hiyo, Bw. Juma Mkomi, Mwinuka amesema kuwa afua za kudhibiti magonjwa hayo zinapaswa kuingizwa katika mipango, bajeti na shughuli za kawaida za Wizara na Taasisi za Umma ili kulinda afya za watumishi na kuongeza ufanisi katika utendaji kazi.
“Afya ya mtumishi ni sehemu muhimu ya mafanikio ya Taasisi. Hivyo, ni wajibu wa kila mwajiri kuhakikisha afua hizo zinatekelezwa kwa vitendo, pamoja na kuimarisha huduma za afya ya akili na kutoa msaada wa kisaikolojia kwa watumishi,” amesema Mwinuka.
Aidha, amewahimiza waajiri kutoa elimu na mafunzo kwa watumishi, huku wakijenga uwezo wa kamati, waratibu na waelimishaji rika wanaohusika na utekelezaji wa afua hizo katika maeneo ya kazi.
Amesema Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora itaendelea kushirikiana na Wizara na Taasisi za Umma kufuatilia utekelezaji wa mikakati hiyo, kutathmini mafanikio yaliyopatikana na kubaini changamoto zinazohitaji ufumbuzi.
Vilevile, amezitaka Wizara kuhakikisha Taasisi za Umma zilizo chini yake zinatekeleza Mwongozo wa Kudhibiti VVU, UKIMWI na Magonjwa Sugu Yasiyoambukiza Mahali pa Kazi katika Utumishi wa Umma wa mwaka 2014, pamoja na kuwasilisha taarifa za utekelezaji kwa wakati.
Ameeleza kuwa uwasilishaji wa taarifa hizo utaiwezesha Serikali kufuatilia maendeleo, kutambua changamoto na kupanga maboresho yatakayosaidia kuimarisha utekelezaji wa afua hizo katika utumishi wa umma.
Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi Msaidizi wa Sehemu ya Anuai za Jamii, ambaye pia ni Afisa Ustawi wa Jamii Mwandamizi, Bi. Juliana Ntukey, amewataka wajumbe wa kikao hicho kushiriki kikamilifu katika majadiliano ili kufikia maazimio yatakayosaidia kuboresha utendaji kazi katika maeneo yao na kuimarisha ustawi wa Taifa.






No comments:
Post a Comment