
Na Okuly Julius, OKULY BLOG, DODOMA
Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dodoma (DUWASA) imebaini wizi wa mita 103 za maji ndani ya kipindi cha miezi mitatu, huku ikionya kuwa vitendo hivyo vinaweza kuongeza gharama za uendeshaji na kuhatarisha miundombinu ya huduma za maji na majitaka jijini Dodoma.
Mkurugenzi Mtendaji wa DUWASA, Mhandisi Aron Joseph, ameyasema hayo Oktoba 26, 2026, jijini Dodoma, akizungumza na waandishi wa habari kuhusu changamoto zinazoikabili mamlaka hiyo, ikiwemo wizi wa mita za maji na mifuniko ya chemba za majitaka.
Amesema wizi huo ni changamoto inayohitaji ushirikiano wa wananchi katika kulinda miundombinu ya maji na usafi wa mazingira, akiwataka kutoa taarifa kwa mamlaka husika wanapobaini vitendo vinavyotia shaka.
Akizungumzia utaratibu wa ufungaji wa mita za maji, Mhandisi Aron amesema Sheria ya Huduma za Maji na Usafi wa Mazingira Na. 5 ya mwaka 2019, pamoja na Kanuni ya 47, inaelekeza mita kufungwa nje ya geti au fensi kwa kushirikiana na mteja.
Amesema utaratibu huo unalenga kuweka mita katika eneo linalofaa na salama, kurahisisha usomaji wake pamoja na kuwezesha wataalamu wa DUWASA kufanya uhakiki bila usumbufu.
Hata hivyo, amesema takribani asilimia 70 ya wateja wa DUWASA jijini Dodoma wana mita zilizofungwa ndani ya fensi, hali inayoweza kuleta changamoto kwa watumishi wanaohusika na usomaji wa mita kila mwezi.
Kutokana na hali hiyo, amewataka wateja ambao mita zao zipo ndani ya fensi kushirikiana na mamlaka kuhakikisha usomaji unafanyika kwa wakati, huku akisisitiza kuwa hakuna mteja anayepaswa kuhamisha au kuingilia mita bila kushirikisha DUWASA ili kuepusha hitilafu.
Katika hatua nyingine, Mhandisi Aron amekemea tabia ya wizi wa mifuniko ya chuma ya chemba za majitaka, akiwataka wananchi kuacha kupokea au kununua mifuniko hiyo kutoka kwa watu wanaoshukiwa kuwa wezi.
Amesema mifuniko hiyo, ambayo baadhi yake ina alama za DUWASA, imetengenezwa kwa chuma kizito ili kuhimili uzito wa magari makubwa yanayopita barabarani na hivyo kuwa sehemu muhimu ya usalama wa miundombinu ya majitaka.
Ameeleza kuwa kuondolewa kwa mifuniko hiyo kunaweza kuacha chemba wazi na kuhatarisha usalama wa watembea kwa miguu, waendesha pikipiki na madereva, pamoja na kusababisha ajali na kuathiri mazingira.
Mhandisi Aron amewataka wananchi kutoa taarifa kwa Jeshi la Polisi au kutumia namba rasmi za dharura za DUWASA wanapobaini au kushuku wizi wa mita za maji na mifuniko ya chemba za majitaka.
Amesisitiza kuwa kulinda miundombinu hiyo ni jukumu la pamoja kati ya mamlaka na wananchi, akieleza kuwa ushirikiano huo utasaidia kuboresha huduma za maji na usafi wa mazingira pamoja na kupunguza uharibifu unaosababishwa na vitendo vya uhalifu.




No comments:
Post a Comment