BoT YAIMARISHA MFUMO WA SEMA NA BoT KULINDA HAKI ZA WATUMIAJI WA HUDUMA ZA FEDHA - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Thursday, November 5, 2026

BoT YAIMARISHA MFUMO WA SEMA NA BoT KULINDA HAKI ZA WATUMIAJI WA HUDUMA ZA FEDHA


Afisa wa Benki Kuu kutoka Kurugenzi ya Ustawi na Huduma Jumuishi za Fedha, Bi. Janeth Kiwia.


Na Okuly Julius, OKULY BLOG, DAR ES SALAAM


Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imeimarisha usimamizi wa haki za watumiaji wa huduma za fedha kupitia mfumo wa kidijitali wa Sema na BoT, unaolenga kurahisisha upokeaji, ufuatiliaji na utatuzi wa malalamiko ya wananchi wanapokumbana na changamoto katika taasisi za fedha.

Mfumo huo ni sehemu ya juhudi za Benki Kuu kuhakikisha watumiaji wa huduma za fedha wanapata njia rahisi, huru na zisizo na gharama za kuwasilisha malalamiko yao, huku wakihakikishiwa haki zao zinalindwa kwa mujibu wa sheria, kanuni na taratibu zilizowekwa.

Akizungumza Novemba 5, 2026 jijini Dar es Salaam, Afisa wa Benki Kuu kutoka Kurugenzi ya Ustawi na Huduma Jumuishi za Fedha, Bi. Janeth Kiwia, amesema BoT ina jukumu la kulinda watumiaji wa huduma za fedha kwa kuhakikisha taasisi zinazosimamiwa na benki hiyo zinatoa huduma kwa kuzingatia haki za wateja.

Kiwia alikuwa akiwasilisha mada kuhusu ulinzi wa watumiaji wa huduma za fedha na utatuzi wa malalamiko kupitia mfumo wa Sema na BoT katika semina ya siku tatu ya waandishi wa habari za uchumi na masoko ya fedha iliyoandaliwa na Benki Kuu.

Amesema utatuzi wa malalamiko unafanyika kwa kuzingatia kanuni na miongozo iliyowekwa mwaka 2019 na 2025, ambayo inaelekeza namna taasisi za fedha zinavyopaswa kupokea, kushughulikia na kutatua malalamiko ya wateja pamoja na wajibu wa Benki Kuu katika kusimamia utekelezaji wake.

Ameeleza kuwa taasisi za fedha zinapaswa kuwa na mifumo madhubuti ya kupokea malalamiko kupitia njia mbalimbali, zikiwemo simu maalumu, barua pepe na madawati ya huduma kwa wateja, ili kuhakikisha wateja wanapata fursa ya kueleza changamoto zao na kupata ufumbuzi.

Katika maelezo yake, Kiwia amebainisha kuwa BoT inasimamia makundi makuu matatu ya watoa huduma za fedha, ambayo ni benki, watoa huduma za mifumo ya malipo na taasisi zinazotoa huduma ndogo za fedha.

Amesema kundi la benki linajumuisha benki za maendeleo (Development Banks), benki za mikopo ya nyumba (Mortgage Banks) na benki za biashara (Commercial Banks), huku watoa huduma za mifumo ya malipo wakijumuisha taasisi zinazowezesha miamala kupitia huduma za fedha kwa njia ya simu na pochi za kielektroniki.

Aidha, amesema watoa huduma za mifumo ya malipo wasio benki (Non-Bank Payment System Providers) wana nafasi muhimu katika kuunganisha mifumo ya malipo kati ya benki na huduma za fedha kwa njia ya simu, hivyo nao ni sehemu ya wigo wa usimamizi wa Benki Kuu.

Amesisitiza kuwa uelewa wa wigo huo ni muhimu kwa wananchi ili wajue taasisi za kuwasiliana nazo wanapokumbana na changamoto za huduma za kifedha, badala ya kupeleka malalamiko katika mamlaka zisizohusika.

Akifafanua kuhusu dhana ya ulinzi wa mtumiaji wa huduma za fedha, Kiwia amesema inahusisha sheria, kanuni, miongozo, taratibu na sera zinazolenga kulinda haki za wateja na kuhakikisha wanapata bidhaa na huduma za fedha kwa usawa.

Amesema mtumiaji anayelengwa katika mfumo huo ni mtu wa mwisho anayetumia huduma za fedha kwa manufaa yake binafsi, tofauti na wakala ambaye hutoa huduma hizo kwa niaba ya taasisi husika.

Aidha, ameeleza kuwa si malalamiko yote yanayohusu sekta ya fedha yapo chini ya Benki Kuu, kwani malalamiko yanayohusu bima, hifadhi ya jamii na soko la mitaji hushughulikiwa na mamlaka nyingine zenye dhamana ya kusimamia sekta hizo.

Kiwia amewahimiza wananchi kuongeza uelewa kuhusu haki zao na mifumo iliyowekwa ya kuwasilisha malalamiko, akieleza kuwa uelewa huo utasaidia kuimarisha uwajibikaji wa watoa huduma za fedha na kuongeza imani ya wananchi katika mifumo ya kifedha nchini.

No comments:

Post a Comment