Na WMJJWM, Rorya Mara
Mkuu wa Wilaya ya Rorya mkoani Mara, Stanslaus Mabula amebainisha kuwa, baadhi ya wazazi wanaendelea kubuni njia mbadala za kutekeleza vitendo vya ukeketaji katika wilaya hiyo, kwa kivuli cha mila, desturi na tamaduni.
Mabula ameyasema hayo wakati akizindua kampeni maalum ya siku tatu ya kutoa elimu na kuzuia vitendo vya ukeketaji wilayani humo, iliyoanza Novemba 06, 2026 katika kijiji cha Nyanchankenye.
Amesema Serikali haitavumilia vitendo hivyo vikiendelea katika Wilaya ya Rorya huku akizitaja baadhi ya kata zinazoendelea kwa vificho.
"Zipo kata ndani ya wilaya yetu ambazo zinaonesha dhahiri viashiria vya vitendo vya ukekeraji hasa Burongo, Nkoyo, Kikoma, Nguribe, Mloche, Nyahongo, Kang'ombe, Nyamagaro, Nyamtinga, Baraki, Kisumwa, Tuliopo, Kigunga, Kinyenche, Nyahunga na Komuge" Amezitaja DC Mabula.
Mkuu wa Wilaya Mabula, ameungana na timu ya wataalamu kutoka Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Ofisi ya Waziri Mkuu TAMISEMI, wahamasishaji wa kitaifa na wadau mbalimbali katika kampeni ya kutokomeza vitendo vya ukeketaji kwa watoto wa kike wilayani humo.
Awali akieleza lengo la kampeni hiyo, mratibu kutoka Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Dennis Mose amesema, Serikali inaendelea kutoa elimu hasa kipindi hiki ambacho watoto wanarudi nyumbani kwa ajili ya likizo.
Naye Afisa Ustawi wa Jamii kutoka Wizara hiyo, Anna Mgelwa akiitaja sheria ya mtoto sura ya 13 kinachokataza ukeketaji kwa mtoto wa kike huku akibainisha kuwa, adhabu ya kifungo cha miaka 5 hadi 15 na faini isiyopungua sh. Milioni 2 na fidia kwa kusababisha madhara.
Kwa upande wake Afisa Maendeleo ya Jamii, kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu TAMISEMI Christopher Mushi amesema kupitia utoaji huo wa elimu kwa njia ya majadiliano, wananchi wanafikia hatua ya kukubaliana na mabadiliko na kuachana na vitendo vya ukeketaji.




No comments:
Post a Comment