WABIA WA MAENDELEO KATIKA SEKTA YA NISHATI (EDPG), WAAHIDI KUENDELEA KUSHIRIKIANA NA SERIKALI MIRADI YA REA - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Friday, November 6, 2026

WABIA WA MAENDELEO KATIKA SEKTA YA NISHATI (EDPG), WAAHIDI KUENDELEA KUSHIRIKIANA NA SERIKALI MIRADI YA REA


Na Mwandishi Wetu - Mafia, Pwani


Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Stanslaus Nyongo ameupongeza Wakala wa Nishati Vijijini (REA) kwa kazi kubwa ya kufikisha umeme vijijini ambapo imekuwa ni chachu kukua kwa viwanda pamoja na uchumi wa wananchi vijijini.


Nyongo ametoa pongezi hizo leo Novemba 6, 2026 Wilayani Mafia wakati akifungua Mkutano wa Pili wa Mwaka kati ya Wabia wa Maendeleo katika Sekta ya Nishati (EDPG) pamoja na REA uliolenga kufanya tathmini ya miradi iliyotekelezwa na wakala huo katika kipindi cha mwaka mmoja.

“Mkoa wa Pwani ni Mkoa wa Maendeleo, ni Mkoa wa viwanda. Viwanda sasa hivi vinajengwa vijijini. Vijijini wanahitaji umeme. Juhudi za Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kuelekea dira ya 2050 pamoja na juhudi za Wabia wa Maendeleo kwa pamoja tumeweza kupeleka maendeleo ya umeme vijijini,’ amesema Mkuu huyo wa Mkoa.


Awali, Katibu Mkuu anayeshughulikia Umeme na Nishati Jadidifu kutoka Wizara ya Nishati, Mhandisi Felchesmi Mramba amesema kuwa Wabia wa Maendeleo wamekuwa mstari wa mbele kuisaidia Serikali kutekeleza miradi mbalimbali ya sekta ya nishati ikiwemo usambazaji wa umeme vijijini, uzalishaji wa nishati jadidifu na usafirishaji wa umeme.


Mwenyekiti wa Bodi ya Nishati Vijijini (REB), Balozi Meja Jenerali (mstaafu), Jacob Kingu amewashukuru Wabia wa Maendeleo kwa mchango wao katika Miradi ya kusambaza nishati vijijini na kuahidi yeye pamoja na Bodi yake kuendelea kuisimamia Menejimenti ya REA kuhakikisha mipango iliyopangwa inafikiwa na fedha zilizotengwa zinatumika kwa malengo yaliyokusudiwa. 


Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa REA, Mhandisi Hassan Saidy amesema pamoja na serikali kufanikiwa kusogeza miundombinu ya umeme katika Vijiji na Vitongoji vingi nchini, Wakala umeweka vipaumbele vitatu vya kimkakati vinavyolenga kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora na kunufaika kiuchumi kwa kuwepo kwa nishati hiyo.

Mhandisi Saidy amevitaja vipaumbele hivyo kuwa ni kuhakikisha wateja wengi zaidi wanaunganishiwa umeme, kuboresha upatikanaji na ubora wa huduma ya umeme kwa kujenga Vituo vidogo vya Kupoza na Kusambaza Umeme pamoja na kuimarisha matumizi ya umeme katika shughuli za uzalishaji mali na kuboresha huduma za kijamii.


Akizungumza kwa niaba ya Wabia hao wa Maendeleo katika Sekta ya Nishati, Dkt. Rhonda Jordan ambaye pia ni Mtaalam Mwandamizi wa Nishati kutoka Benki ya Dunia, amesisitiza kuwa wataendelea kushirikiana na Serikali kupanua huduma za nishati zilizo salama, za uhakika na endelevu illi kufanikisha malengo ya nchi katika sekta ya nishati.

No comments:

Post a Comment