Na Mwandishi Wetu- Dar es Salaam
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Mwingulu Nchemba, anatarajiwa kuwa Mgeni Rasmi katika Kilele cha Maadhimisho ya Kitaifa ya Siku ya Watu wenye Ulemavu Duniani kwa Mwaka 2026 itakayofanyika katika Viwanja vya Nyamagana, mkoani Mwanza tarehe 03 Desemba 2026.
Hayo yamesemwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Uratibu na Watu Wenye Ulemavu Prof. Palamagamba Kabudi (Mb.) wakati akizungumza na waandishi wa habari leo Novemba 28, 2026 kuhusu Maadhimisho ya Siku Ya Watu Wenye Ulemavu Duniani kwa Mwaka 2026
Amesema, katika kilele cha Maadhimisho hayo, Serikali imepanga kuzindua nyaraka nne muhimu zinazolenga kuimarisha utekelezaji wa haki za Watu wenye Ulemavu, kuboresha mifumo ya utoaji wa huduma na kuhakikisha kuwa mahitaji yao yanazingatiwa katika mipango na programu mbalimbali za maendeleo.
“Nyaraka hizo ni Mwongozo wa Kitaifa wa Viwango vya Ufikivu kwa Watu wenye Ulemavu wa Mwaka 2026 ulioandaliwa na Ofisi ya Waziri Mkuu kwa lengo la kuweka viwango na maelekezo yatakayozingatiwa katika kuhakikisha kuwa majengo, miundombinu, usafiri, taarifa, mawasiliano na huduma mbalimbali zinakuwa fikivu kwa Watu wenye Ulemavu” ameeleza Prof. Kabudi.
Aidha, amebainisha nyaraka nyingine ni Mwongozo wa Kitaifa wa Usimamizi wa Mashauri ya Watu wenye Ulemavu wa Mwaka 2026 ulioandaliwa kwa lengo la kuweka mfumo wa pamoja wa kutambua, kupokea, kutathmini, kushughulikia, kuratibu na kufuatilia mashauri yanayohusu watu wenye Ulemavu na unatarajiwa kuimarisha uwajibikaji na ushirikiano kati ya taasisi zinazotoa huduma, kuwezesha utoaji wa rufaa na kuhakikisha kuwa Watu wenye Ulemavu wanapata huduma stahiki kwa wakati na kwa kuzingatia mahitaji yao.
Vilevile, utazinduliwa Mpango Kazi wa Kuimarisha Usawa katika Upatikanaji wa Huduma za Afya kwa Watu wenye Ulemavu wa Mwaka 2026–2031 unaolenga kuimarisha upatikanaji wa huduma bora, salama na jumuishi za afya kwa Watu wenye Ulemavu kwa kuondoa vikwazo vya kimazingira, kimawasiliano, kitaasisi na kimtazamo vinavyoweza kuzuia upatikanaji wa huduma hizo.
Pia, ripoti kuhusu Hali Halisi ya Watoto na Vijana wenye Ulemavu Tanzania ya Mwaka 2026 ni nyaraka nyingine itakayozinduliwa ikiwa na lengo la kutoa taarifa na ushahidi kuhusu hali ya watoto na vijana wenye ulemavu nchini, ikijumuisha fursa, changamoto na vikwazo wanavyokabiliana navyo katika kupata elimu, huduma za afya, ulinzi, mafunzo ya ujuzi na kushiriki katika shughuli za maendeleo.
“Uzinduzi wa nyaraka hizi ni sehemu ya juhudi za Serikali za kuimarisha mifumo ya kisera, kitaasisi na kiutendaji katika kushughulikia masuala ya Watu wenye Ulemavu, Nyaraka hizi zinakamilishana kwa kuzingatia maeneo muhimu ya ufikivu, usimamizi wa mashauri, upatikanaji wa huduma za afya na matumizi ya takwimu na ushahidi katika kuboresha huduma kwa watoto na vijana wenye ulemavu” amebainisha Prof. Kabudi.
Sambamba na hilo, Prof Kabudi ametoa wito kwa Wizara, Idara na Taasisi za Serikali, Mamlaka za Serikali za Mitaa, sekta binafsi, Vyama vya Watu wenye Ulemavu na wadau wengine kujiandaa kutumia nyaraka hizo katika mipango na shughuli zao mara zitakapozinduliwa. Aidha, serikali itaendelea kusimamia na kuratibu utekelezaji wake ili kuhakikisha kuwa nyaraka hizo zinakuwa nyenzo za kuleta mabadiliko chanya katika maisha ya Watu wenye Ulemavu nchini.
Maadhimisho ya Kitaifa ya Siku ya Watu wenye Ulemavu Duniani kwa Mwaka 2026 yameandaliwa na Ofisi ya Waziri Mkuu – Sera, Bunge, Uratibu na Watu wenye Ulemavu kwa kushirikiana na Shirikisho la Vyama vya Watu wenye Ulemavu Tanzania (SHIVYAWATA) na yanafanyika katika Viwanja vya Nyamagana mkoani Mwanza, kuanzia tarehe 27 Novemba hadi 03 Desemba 2026 ambapo Serikali imeandaa maadhimisho hayo kwa lengo la kuendelea kuongeza uelewa wa jamii kuhusu haki za Watu wenye Ulemavu, kutathmini mafanikio yaliyopatikana na kuhamasisha ushiriki wao katika shughuli za maendeleo.





No comments:
Post a Comment