Na Mwandishi Wetu - Rufiji
Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST), Mha. Ally Samaje, ameipongeza timu ya wataalamu wa jiolojia wa GST wanaofanya utafiti wa madini katika Wilaya ya Rufiji kwa kujituma, kufanya kazi kwa bidii na kuonesha dhamira ya dhati katika kutekeleza majukumu yao, hatua inayochangia maendeleo ya sekta ya madini nchini.
Pongezi hizo amezitoa wakati wa ziara ya sehemu ya uwakilishi wa Menejimenti ya GST ya kukagua shughuli za utafiti wa kijiolojia zinazoendelea katika maeneo ya QDS Na. 239 na 240, yanayogusa Wilaya za Rufiji na Kilwa, ambapo amekutana na watumishi hao na kujionea maendeleo ya zoezi hilo.
QDS hizo ni miongoni mwa QDS tisa zilizokuwa zimebaki bila kuwa na ramani ya jiolojia kati ya QDS 322 zilizopo nchini. Hivyo, kukamilika kwa QDS hizo kutafanya kubaki QDS saba tu ambazo hazina ramani ya jiolojia, na hivyo utafiti wa jiolojia kufikia takribani asilimia 97.8.
Akizungumza na watumishi hao, Mha. Samaje amesema amefarijika kuona namna wataalamu hao wanavyojitoa katika kutekeleza majukumu yao kwa bidii na kujituma, akieleza kuwa hali hiyo ni ishara chanya ya mchango wao katika kuendeleza sekta ya madini nchini kupitia tafiti za kijiolojia.
Amesisitiza kuwa kazi inayofanywa na wataalamu hao ni muhimu kwa Taasisi na Wizara kwa ujumla, kwani matokeo ya tafiti hizo yatatoa taarifa za kitaalamu zitakazowasaidia Watanzania na wawekezaji wa ndani na nje ya nchi kufanya shughuli za uchimbaji wa madini kwa kutumia taarifa sahihi za kijiolojia, badala ya kutegemea kubahatisha, hivyo kuongeza uwezekano wa kupata matokeo yenye tija.
Aidha, amesema uongozi wa GST unatambua umuhimu na ukubwa wa kazi inayofanywa na wataalamu hao na uko tayari kuendelea kutoa ushirikiano unaohitajika ili kuhakikisha shughuli za utafiti zinaendelea vizuri bila kukwama, huku akibainisha kuwa Taasisi imewezeshwa kifedha kutekeleza tafiti hizo katika maeneo mbalimbali nchini kupitia fedha zinazotengwa katika Mfuko Maalumu wa Utafiti wa Madini.
Kutokana na hali hiyo, amewahimiza watumishi hao kuwa tayari kuendelea kutekeleza shughuli za utafiti katika maeneo mengine yatakayopangwa, sambamba na kujiendeleza kwa kuongeza uelewa kuhusu shughuli mbalimbali zinazofanywa na Taasisi ili kuboresha utendaji wao, kuongeza ufanisi na kuwa bora zaidi katika nafasi zao za kazi.
Naye Mjiolojia kutoka GST, Bw. Joseph Baraka Nyamullo, ameomba Taasisi kuongeza vitendea kazi vinavyohitajika katika shughuli za utafiti ili kuwawezesha wataalamu kufanya kazi kwa ufanisi na kupata mazingira bora ya kufanyia kazi wanapokuwa katika maeneo ya utafiti, ambayo mengi yako porini na mbali na makazi ya watu.
Kwa upande wa maendeleo ya utafiti, zoezi hilo limefikia asilimia 40 ya utekelezaji wake, huku maeneo yanayofanyiwa utafiti yakijumuisha Utete, Nyamwage na Ruhoi wilayani Rufiji, pamoja na Somanga katika Wilaya ya Kilwa.






No comments:
Post a Comment