NA SHUA NDEREKA, OKULY BLOG, MOROGORO
Joyce Shebe ameibuka mshindi wa uchaguzi wa Makamu Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), baada ya kupata kura 88 na kumshinda mgombea mwenzake Salome Kitomali aliyepata kura 53, katika uchaguzi uliofanyika kuziba nafasi hiyo.
Uchaguzi huo umefanyika mkoani Morogoro, kufuatia aliyekuwa Makamu Mwenyekiti wa jukwaa hilo, Bakari Machumu, kupata majukumu mengine ya kiserikali.
Akitoa matokeo ya uchaguzi huo, msimamizi wa uchaguzi Dk. Frank Sanga, amesema jumla ya wajumbe 141 walipiga kura, ambapo uchaguzi huo ulikuwa huru na wa haki na ulizingatia kanuni zote kwa mujibu wa Katiba ya TEF.
“Mbali na kura hizo ambazo wajumbe wamepiga kuwachagua wagombea, kura zilizoharibika ni sifuri,” amesema Dk. Sanga.
Akizungumza mara baada ya kutangazwa mshindi, Joyce Shebe amesema licha ya kuondoka katika chumba cha habari cha Clouds, ameendelea kujishughulisha na uandishi wa habari pamoja na kuwa mwanachama wa TEF, akiahidi kuendelea kulitumikia jukwaa hilo kwa uaminifu.
Pia, Salome Kitomali amewashukuru wajumbe wote waliompigia kura na hata wale ambao hawakumchagua.
Naye Bakari Machumu amesema, ataendelea kushirikiana na wahariri pamoja na uongozi wa TEF, akisisitiza kuwa majukumu yake mapya hayamkatishi uhusiano wake na taaluma ya uandishi wa habari.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Jukwaa la wahariri Tanzania (TEF), Deodatus Balile, amempongeza Joyce Shebe kwa ushindi huo, huku akizitaka taasisi nyingine kuiga mfano wa TEF katika kusimamia uchaguzi huru na wa haki, akieleza kuwa matokeo yaliyokuwa ndani ya sanduku la kura ndiyo yaliyotangazwa.



No comments:
Post a Comment